XXXXXXXXXXXX
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amekemea tabia ya baadhi ya watu wenye ulemavu kutumia hali waliyonayo kupita barabarani na kuomba pesa kwa wapita njia wakati wanao uwezo wa kufanya kazi na kujiingizia kipato.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa wilaya Kigoma alisema kuwa ulemavu siyo tatizo la kufanya watu wakashindwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kujiingizia kipato.
Pamoja na hilo Mkuu huyo wa mkoa amewataka maafisa maendeleo ya jamii katika halmashauri kuhakikisha wanatumia nafasi yao kuwafikia watu wenye ulemavu kwa kuwaandikia maandiko ya michanganuo ya miradi na kuwafundisha namna ya usimamizi endelevu wa miradi ili miradi watakayofanya iwe na tija na kubadilisha maisha yao.
“Serikali imeweka mifumo ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa namna mbalimbali ikiwemo kutenga fedha za mikopo kwenye halmashauri hivyo ni wazi watu wenye ulemavu wanayo fursa ya kuifikia mikopo hiyo kwa makundi au mtu mmoja mmoja na kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kupita mitaani kuomba omba kwa kigezo cha ulemavu wao,”Alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya Kigoma, Esther Mahawe alisema kuwa ofisi yake imeshatoa maelekezo kwa halmashauri kuhakikisha fedha kwa ajili ya mikopo kwa walemavu inatolewa pamoja na mafunzo na kwamba imekuwa ikifanyika hivyo kila wakati kwa halmashauri ya wilaya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akitoa maelezo kuhusu hafla ya chakula iliyoandaliwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu alisema kuwa imelenga kujumuika pamoja na watu hao katika kuelekea sherehe za mwisho wa mwaka ili kuwaonyesha upendo na kusherehekea kama ambavyo watu wengine wanasherehekea sikukuu hizo za mwisho wa mwaka.
Mkuu huyo wa wilaya Kigoma alisema kuwa zaidi ya watu wenye ulemavu 700 wamehudhuria hafla hiyo ya chakula ambapo pamoja na chakula walichokula pamoja pia walipewa chakula ambacho wataenda kupika nyumbani na hiyo ni kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu.
Baadhi ya watu wenye ulemavu waliohudhuria hafla hiyo akiwemo Paschal Saidi wameeleza kufurahishwa na kusanyiko hilo la watu wenye ulemavu ambalo linawawezesha kukusanyika na kufurahi pamoja na watu wengine.
Saidi alisema kuwa kusanyiko hilo limekuwa na faida kwao kwani hotuba na mambo yanayosemwa na viongozi yanawapa faraja kuona namna ya kukabiliana na hali zao lakini pia kusanyiko hilo linawapa nafasi kukutana na viongozi na kuzungumza mambo na changamoto zinazowahusu.
0 Comments