Header Ads Widget

MKUU WA WILAYA NAMTUMBO AWATAKA WANANCHI KUACHA TABIA YA KUWAFICHA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU

 Na Amon Mtega, Namtumbo

MKUU wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dkt Julius Ningu amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye mahitaji maalumu (Walemavu)kwa kuwa kufanya hivyo kunawafanya watoto huo kukosa haki zao za msingi ikiwemo kupatiwa Elimu.


Ningu ametoa wito huo wakati akipokea msaada wa viti mwendo viwili (Wheel chair)na mashine moja ya alama nundu kutoka kwenye kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambavyo vimegharimu zaidi ya kiasi cha shilingi Milioni nne.

Mkuu huyo akipokea vifaa hivyo kutoka kwenye kampuni hiyo ambavyo vimeenda sambamba na miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania kisha kuwakabidhi wahitaji hao amesema kuwa bado kumekuwepo na baadhi ya wazazi kuwaficha watoto wao wenye mahitaji maalumu jambo ambalo halikubaliki.


 Dkt Ningu amesema kuwa kuanzia sasa ofisi yake  itaanza kufuatilia wazazi ambao wanaendelea kuwaficha watoto wenye mahitaji hayo kwa kutumia takwimu za Sensa  iliyofanywa mwaka huu.


 Hata hivyo mkuu huyo ameishukuru kampuni ya Mantra kwa msaada huo ambao  utawasaidia wanafunzi hao katika kuwapunguzia changamoto ambazo walizokuwa wakikutana nazo.

 Kwa upande wake mkurugenzi muendeshaji wa kampuni ya Mantra inayojishughulisha na madini ya urani katika Wilaya hiyo Alexander Ryabchenko amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika kutatua changamoto za wahitaji.

Naye meneja uendelevu wa mradi katika kampuni ya Mantra Majani Wambura amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI