Header Ads Widget

MAJI YA BOMBA TOKA ZIWA VICTORIA YAANZA KUTOKA KIJIJI CHA CHITARE

 

Na Shomari Binda-Musoma

BAADA ya wananchi wa Kijiji cha Chitare Kata ya Makojo Jimbo la Musoma vijijini kusubiri zaidi ya miaka 9 kupata maji hatimaye wameanza kuyapata. 


Mradi wa maji ya bomba kwenye Kijiji hicho na vijiji vingine vya Kata ya Makojo ulianza mwaka wa fedha 2013/2014 na kutekelezwa na halmashauri ya wilaya ya Musoma kwa fedha za miradi ya maji ya serikali na umekuwa ukisuasua.


Wakizungumza wakati wakichota maji kutoka kwenye mabomba, wananchi wa Kijiji hicho wameishukuru serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa kupata huduma ya maji. 

Wamesema wamekuwa wakipata maji kwa kuyafuata ziwani na kukumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo kukutana na wanyama wakali kama mamba na kudhuliwa huku wengine wakipoteza maisha. 


Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mukama Magesa,amesema hiyo ni neema kwao kwa kupata maji ambayo ni uhai kwa binadamu. 


Amesema kwa miaka mingi wameuona mradi huo kwenye Kijiji chao lakini umekuwa hautoi maji lakini kwa sasa wanayapata kwa muda wote. 


Magesa amesema serikali imefanya kazi kubwa ambayo inastahili kupongezwa pamoja na ufatiliaji wa karibu uliofanywa na mbunge wa jimbo la Musoma vijijini, Profesa Sospeter Muhongo.

Mhandisi kutoka ofisi ya Ruwasa wilaya ya Musoma, Innocent Edward, amesema kukamilika kwa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1 utawanufaisha wananchi 8500.


Amesema bado kazi inaendelea kufanyika katika Kata ya Makojo katika mradi wa maji ili vijiji vingine vya Makojo na Chimati viweze kupata maji safi na salama.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS