Bi. Sikitiko Casian Mapunda, Mkazi wa Nguvu Mpya Jijini Dar Es Salaam amemtaja Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Kiongozi na Mama jasiri na shujaa, akimshukuru kwa kuwekeza katika masuala ya Kijamii ikiwemo yanayowahusu wanawake pamoja na watoto.
Bi. Mapunda amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Disemba 15, 2025, akisema huko nyuma baadhi ya Makundi yalisahaulika ikiwemo wanawake na Vijana, akisema ni mara ya kwanza kuona Rais akiwaita Vijana na kuwasikiliza kero na changamoto walizonazo.
"Nimshukuru pia sana Mama kwa namna alivyoifanya miundombinu ya GongolaMboto kupitika tofauti kabisa na zamani ilivyokuwa. Sasa hivi barabara ya Gongolamboto ni tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka mitano iliyopita, ni kama barabara za Ulaya, tuna Mahospitali na mpaka barabara za ndani nazo zinapitika wakati wote." Amesema Bi. Mapunda.
Amemshukuru Rais Samia pia kuhusu usimamizi wake wa mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kwaajili ya wanawake, Vijana na wenye ulemavu, akimuomba pia kushughulikia masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine Bi Mapunda pia akizungumza na mwandishi wetu wa habari, ameeleza na kushukuru kupungua kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini ikiwemo matukio ya ubakaji kwa wasichana na wanawake, akisema huko nyuma kabla ya ujio wa Rais Samia udhalilishaji ulikuwa mkubwa na wanawake wengi wa Mijini na Vijijini walikuwa na hofu kubwa ya kupita katika baadhi ya maeneo kwa kuhofia matukio ya ubakaji yaliyokuwepo.






0 Comments