Header Ads Widget

JENIFA, MSINGI WA UJASIRIAMALI NI WAZO NA SIO FEDHA, FEDHA INAKUJA KUTEKELEZA WAZO.

NA CHAUSIKU SAID, MATUKIO DAIMAAPP MWANZA

Wahitimu wa chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Mkoani Mwanza wametakiwa kufanya upembuzi yakinifu wa mawazo ya kibiashara waliyonayo ili kuweza kuyatekeleza kwa ufanisi.


Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu kuu wizara ya fedha na Mipango Jenifa Omolo  alipomwakilisha Waziri wa fedha Dkt, Mwigulu Nchemba kwenye Duru ya pili ya mahafali ya 36 ya chuo hicho Mkoani hapa na kueleza kuwa serikali iko tayari kuwasaidia vijana wenye mawazo chanya ya kibiashara ili kutimiza malengo yao.

Jenifa ameeleza kuwa wahitimu hao wanapaswa kuwa na moyo wa kuthubutu kufanyia kazi maono yao na kutoogopeshwa na watu wachache waliokuwa na maono kama yao lakini wakashindwa.


"Wengi waliofanikiwa kwenye biashara ni wale waliojaribu mara kadhaa bila kuchoka hadi wakafanikiwa hivyo nanyi msichoke," Jenifa.


Hata hivyo ameendelea kuwaasa wahitimu hao kujiunga katika makundi na kuyasajili ili yatambulike rasmi na kuweza kupata fursa katika ununuzi unaofanywa na serikali.

"Vile vile ninapenda kuwahimiza wahitimu wetu na wanafunzi wanaendelea na masomo kuchangamkia fursa ya upendeleo inayotolewa na sheria ya ununuzi wa umma sura 410 Kwa makundi maalumu katika jamii hususani vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu" Alisema Jenifa.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa chuo hicho Profesa Martha Qorro ameeleza kuwa wamekuwa wakitoa elimu ambayo itawasaidia wahitimu hao watakapokuwa wanafanya kazi zao huku jamii ikiwa imewazunguka.


"Kwanza wahitimu hawa wanamazowea ya kukaa na wananchi kutokana na elimu waliyoipata wanaweza kuishi mazingira yeyote na kufanya kazi," Alisema Martha.


Profesa Hozen Mayaya ni Mkuu wa Chuo Cha  Mipango amesema kuwa takribani wahitimu 8,916 wanaume wakiwa 3,922 na wanawake 4,994 ambao wamefundishwa na kupata uelewa na kuwa nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi stahiki .

Mayaya ameeleza kuwa serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika maswala ya elimu hapa Nchini Kwa kuweka miundombinu salama kwa taasisi za elimu ya juu, na shule za Sekondari Kwa  kufanya ukarabati.


"Sera ya elimu bure sasa ni kuanzia chekechea hadi kidato Cha sita, pamoja na bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imeongezeka na kufanya idadi ya wanufaika kuwa wengi zaidi"Alisema Mayaya.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS