XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wananchi wa kata ya Njombe mjini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwasikiliza wagombea wa nafasi ya udiwani wanaonadi sera zao ili kupata ridhaa ya kuongoza kata hiyo kwenye uchaguzi wa marudio utakaofanyika hapo desemba 17 mwaka huu.
Asasi ya kiraia ya Umbrela of Women and Disabled Organization[UWODO] chini ya mkurugenzi wake Hamis Kassapa ilipewa dhamana ya kuelimisha wananchi ambapo inasema licha ya kampeni hizo kuanza tangu desemba 12 mwaka huu lakini mwitikio wa wananchi kujitokeza kusikiliza sera za wagombea kwenye mikutano ya kampeni umekuwa mdogo.
Wakati kampeni zikiendelea katika mitaa ya kata hiyo tayari tume ya uchaguzi imeshawaapisha wasimamizi wa uchaguzi huo wapatao 248 watakaosimamia vituo 62 kwa mujibu wa mratibu wa uchaguzi jimbo la Njombe mjini KENANI MALIGA.
Wagombea wa nafasi ya udiwani kata ya njombe mjini kutoka vyama vya CCM, ALATANGA NYAGAWA na ACT Wazalendo ALLY MHAGAMA wanaoendelea na kampeni wamekuwa wakitoa ahadi za kuleta maendeleo ikiwemo kwenda kuleta suluhu ya tatizo kubwa la uhaba wa maji katika mji wa Njombe.
Aidha MHAGAMA amesema haiwekezekani Njombe kukawa na vyanzo vingi vya maji lakini wakazi wake wakawa wanapata maji kwa mgao hivyo kama mgombea wa ACT Wazalendo akipata nafasi hiyo atakwenda kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika mkubwa.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Njombe mjini akiwemo REGINAL MWAPINGA na MASHAKA LULAMBO wamesema upo umuhimu mkubwa wa kupata elimu ya haki ya kushiriki katika uchaguzi huo kwani itawasaidia kumjua mgombea sahihi atakaye waletea maendeleo.
Wamesema tume ya uchaguzi kupitia Asasi za kiraia inapaswa kuongeza nguvu katika kutoa elimu hiyo inayoweza kuwasaidia kufahamu umuhimu wa kwenda kusikiliza sera za wagombea kwenye kampeni za uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Disemba 17 mwaka huu.
Uchaguzi huo wa marudio unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo ROMANUS MAYEMBA aliyefariki mwaka 2021 akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
0 Comments