Wamiliki wa Maduka ya Dawa na Vifaa Tiba wametakiwa kutouza bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.
Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TDMA) Kanda ya Mashariki Angelo Malifa wakati wa kuteketeza bidhaa ambazo hazifai kwa matumizi katika kituo cha Waste Management Plant (TMHS) kilichopo Tindwa Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani.
"Mamlaka imeteketeza dawa na vifaa tiba ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu vyenye thamani ya shilingi milioni 56.8 ambavyo vilikamatwa baada ya ukaguzi,"alisema Malifa.
Alisema kuwa bidhaa hizo ambazo zilizoteketezwa zilikamatwa maeneo mbalimbali baada ya kaguzi kufanywa ambapo bidhaa za dawa zina thamani ya shilingi milioni 39.4 na vifaa tiba vina thamani ya shilingi milioni 17.4.
"Katika kutekeleza jukumu hilo Mamlaka hufanya kaguzi maalum na kawaida katika maeneo yote ya mipaka na katika soko la Tanzania Bara kwenye maeneo yanayojihusisha na biashara za dawa, vitendanishi, vifaa, tiba na bidhaa za tumbaku,"alisema Malifa.
Aidha alisema kuwa walibaini uwepo wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi katika soko ambapo zilikutwa zina ubora duni, kutokuwa na usajili wa TMDA na zingine zikiwa zimeisha muda wa matumizi.
0 Comments