NA TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera.
CHAMA cha watu wenye ualbino Kagera (TAS) kimelaani vitendo vya kikatili dhidi watu wenye ualbino yakiwemo mauaji ya watu hao ambayo yameonekana kuanza kushamiri.
Hayo yamesemwa na katibu chama cha watu wenye ualbino Bukoba (TAS) mkoani Kagera , Florence Felician katika mahojiano maalum na chombo hiki, ambapo amesema kuwa jamii inatakiwa kuachana na imani potofu na kuthamini utu.
"Kiukweli inasikitisha na inahuzunisha pia kwa sababu hii hali tulikuwa tumeishaanza kuisahau kutokana na kipindi cha nyuma hali ilivyokuwa, hali ilikuwa imeishakuwa nzuri tushaanza kuishi kwa amani lakini sasa hivi hii hali imeanza kujirudia tena watu wenye ualbino wameanza kuuawa tena kwa kweli inaumiza, jamii inatakiwa kuacha imani potofu kama hizi huwezi kupata utajiri au kupanda cheo kupitia njia kama hizi"
Ameongeza kuwa, jamii inatakiwa kuwapokea watu wenye ualbino na kukaa nao kwa upendo huku akiiomba serikali kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino na kuhakikisha wanatokomeza vitendo hivyo ili kuwasaidia watu hao kuishi kwa amani.
"Watu tumtegemee Mungu kwa kila tunachokifanya, tukubaliane na hali kama wewe ni mfanyabiashara kubaliana na hali, kuwa na imani katika kazi na uipende kazi yako, mafanikio yatakuja sio kuwaza kwenda kwa waganga ukidhani utafanikiwa,jamii ibadilike"
Sambamba na hilo amewaomba watu wenye ualbino nchini kuishi kwa tahadhari na wasisite kutoa taarifa kwa mamlaka zilizo karibu nao wanapogundua kuna hali hawaielewi katika maeneo yao wanapoishi au wanapofanyia kazi.
0 Comments