Na fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kiwango cha uzalishaji umeme kimepungua kwa megawati 300 hadi 350 kutokana na ukame na kupelekea vyanzo vya kuzalisha umeme kukosa maji hali inayochangia ukosefu wa umeme wa uhakika kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Maharage Chande amesema Shirika hilo limekuwa na Mipango ya muda mrefu na mfupi katika kukabiliana na hali hiyo.
Amesema kuwa, kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kinatarajiwa kuongezeka kwa wastani wa Megawati 220 ifikapo katikati ya Disemba na hivyo kupunguza changamoto ya mgao wa umeme uliopo kwa sasa.
Amesema kuwa, kwa asilimia kubwa hali ya upungufu wa umeme uliopo nchini umetokana na uwepo wa changamoto ya uwepo wa ukame pamoja na matengenezo ya miundombinu ya usafirishaji umeme inayofanywa na Shirika hilo.
"Ukame uliopo na matengenezo tunayoendelea kuyafanya ndio yanachangia upungufu wa umeme na hivyo kusababisha umeme kuwa wa mgao" amesema Chande
Ameongeza kuwa, changamoto hizo ndizo zimelifanya shirika hilo kushindwa kuwahudumia wateja wake kwa kiwango kilichokusudiwa, hivyo wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo ambapo hadi kufikia Disemba itakua imeimarika.
Hata hivyo, amesema usambazaji wa umeme kwa kituo cha Kihansi kinachozalisha megawati 180, lakini kwa sasa kutokana na hali ya ukame kinazalisha wastani wa Megawati 17 hadi 30, kikipoteza jumla ya megawati 63 kutokana na upungufu huo wa maji.
Ameongeza kuwa ili kukabiliana na hali hiyo pamoja na mambo mengine yanayoendelea pia wanafanya maboresho ya mashine zake za ufuaji umeme kikiwemo kituo cha Ubungo 3 kinachotarajiwa kuingiza Megawati 20 katika gridi ya Taifa ndani ya siku mbili na zingine 20 mwanzoni mwa Desemba hivyo.
"Kituo cha Kidatu chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50, matarajio ifikapo wiki ijayo Kituo cha Kinyerezi 1 ifikapo mwisho wa mwezi huu kitatoa Megawati 90 ambazo zitaingizwa katika mfumo hivyo hivyo kwa pamoja kufanya jumla ya Megawati 220 kuingizwa katika gridi ya Taifa ifikapo kati kati ya Desemba.
0 Comments