IMEELEZWA kuwa kutokana na matumizi holela ya dawa hasa dawa za aina ya antibaiotiki ni hatari na huweza kuathiri binadamu kutokana na kula mabaki ya dawa hizo kwenye vyakula vinavyotokana na wanyama na kuwa tatizo hilo kubwa linaloikabili dunia kwa sasa na wafugaji wanapaswa kuzingatia ushauri unaotolewa ili kulidhibiti tatizo hilo kwani inakadiriwa kwamba kufikia mwaka 2030 watu zaidi ya milioni 10 watakufa kila mwaka kutokana na dawa kushindwa kuwatibu kwani vimelea vya magonjwa vitakuwa vimejenga usugu .
Hay yamesemwa na Dkt.Qwari Bura ambae ni meneja wa wakala wa maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Leo mjini Iringa wakati akitoa taarifa ya TVLA kuelekea maadhimisho ya miaka 10 toka kuanzishwa kwake .
Alisema kuwa Katika kuadhimisha miaka 10 ya tangu kuanzishwa kwa wakala wamepanga kutoa chanjo za bure kwa wafugaji watakaohudhuria kwenye mikutano na kutolewa kwa wataalamu kwa kushishirikana na mamlaka za serikali za Mitaa yaani halmashauri.
"Chanjo itakayotolewa ni Chanjo ya ugonjwa wa Mdondo Chanjo stahimilivu joto ambayo inaweza kuhifadhiwa bila jokofu kwa siku saba kama haijafunguliwa kwa maeneo yenye joto kama Kyela Mbarali, Ruaha Mbuyuni, Migori na Mkoa wote wa Ruvuma. Kwa maeneo yenye baridi kama Njombe, Mafinga, Tukuyu na Mbeya, chanjo hii inaweza kukaa bila jokofu hadi siku 10 kama haijafunguliwa na ikifunguliwa katika hali yoyote ile inatakiwa itumike ndani ya siku 2 ukilinganisha na chanjo zingine ambazo zikifunguliwa zinatakiwa zitumike ndani ya masaa mawaili tu"
Kwani chanjo hiyo ya Mdondo inayozalishwa na Wakala wao ni Mkombozi wa wafugaji wa maeneo yote yaani mijini ambako kuna umeme wa kuwasha jokofu na maeneo ya vijijini ambako hakuna umeme wa kuwasha jokofu ili kutunza chanjo.
Aidha kuchanja mifugo ni jambo la msingi sana kwa sababu takwimu zinasema asilimia 70 ya magonjwa yanayoambukiza binadamu inatokana na wanyama, maana yake wanyama wakichanjwa kwa kufuata utaratibu uliwekwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, maambukizi ya magonjwa kwa binadamu yatapungua kwa asilimia kubwa hatimaye nchi itakuwa na watu wenye afya bora wenye uwezo wa kuijenga taifa.
"Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ni Wakala ya Serikali chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyoanzishwa kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 245 (iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2009) na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 9 Machi 2012. Wakala ilizinduliwa rasmi tarehe 11 Julai, 2012 na Katibu Mkuu Kiongozi. Wakala hii ilitokana na kuunganishwa kwa iliyokuwa Maabara Kuu ya Mifugo (CVL), Vituo vya Kanda vya Uchunguzi na Utambuzi wa Magonjwa ya Mifugo (VICs), Taasisi ya Utafiti wa Ndorobo (TTRI) Tanga na Kituo cha Utafiti wa Ndorobo (TTRC) Kigoma."
Hivyo wakala ikaamua kufanya maadhimisho ya miaka hiyo 10 tangu ilivyoanzishwa kwa kutenga siku tano kuanzia leo NOvemba 21 mwaka 2022 hadi Novemba 25 mwaka huu kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwa na lengo la kuwafikia wafugaji na kurudisha kile ilichokipata kwa jamii. Maadhimisho haya yatafanyika nchi nzima kwenye vituo vyote vya Makao Makuu na vituo 11 vya mikoani, na kila kituo kimepanga kufanya shughuli mbalimbali katika siku hizo tano kama ifuatavyo:
Alizitaja shughuli zitakazofanyika kuwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusiana na huduma zinazotolewa na TVLA
Kufanya upimaji wa magonjwa ya Mifugo (Bure) kwa maeneo yatakayobainishwa
Uchanjaji wa Mifugo (Bure) kwa maeneo yatakayobainishwa,Utoaji wa Elimu ya Mifugo (Bure),kufanya Ufunguzi wa Jengo Jipya la Maabara na Ofisi Kituo cha Iringa pamoja na
Kutembelea vituo vya watoto yatima na kutoa misaada,kwa upande wa Kituo cha Iringa kinachohudumia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma, tumepanga kufanya yafuatayo.
Hivyo Dkt Bura alisema kuna umuhimu mkubwa katika kupima na kujua ugonjwa unaomsumbua mnyama ili kuweza kutoa tiba sahihi kwani hii itasaidia kuondoa tatizo la kutibu kwa majaribio jambo ambalo hupelekea mfugaji kutumia dawa aina nyingi zinazoweza kupelekea kujenga usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa Kwa hiyo wafugaji wanapaswa kuacha mara moja kutibu wanyama wao bila vipimo ili kulinda afya ya wanyama na binadamu.
Mwisho






0 Comments