Na Gift Mongi,Matukio DaimaAPP
Moshi
Mbunge wa jimbo jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi amesema shahada ya juu ya heshima aliyotunukiwa rais Dkt Samia Suluhu Hassan na chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)hii leo imekuja kwa kuchelewa kwani alistahili mapema zaidi.
Prof Ndakidemi amesema kwa kipindi kifupi alichokaa madarakani kama rais ipo miradi mingi iliyokuwa sugu katika jimbo lake lakini imeweza kupatiwa ufumbuzi wakudumu na kuwa heshima aliyopewa sio kwa bahati mbaya ila anastahili.
Ameitaja baadhi ya miradi hiyo ambayo ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo kwa kipindi kirefu wananchi wake walikuwa wakienda kupata matibabu nje ya wilaya hiyo.
Amesema miradi mingine ni ujenzi wa barabara ikiwemo ile ya Kiboriloni hadi Kidia ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami lakini pia maeneo mengine barabara zimeendelea kujengwa jambo linalopelekea jimbo nzima kuwa na mawasiliano kwa wakati wote.
Hali kadhalika miradi ya maji hususan kata ya Mabogini ambayo wananchi wake walikuwa hawana uhakika wa maji safi na salama sambamba na wakazi wa kata ya Mbokomu huku wakazi wa kata ya Kimochi nao wakipata maji baada ya kutaabika kwa kipindi kirefu.
Kwa mujibu wa mbunge huyo ni kuwa madarasa yameendelea kujengwa sambamba na vituo vya afya hivyo kwa upande wake anaona miradi mingi imetekelezwa kwa kipindi kifupi jambo ambalo halijawahi kutokea.
Prof Ndakidemi amesema shahada hiyo aliyopewa mheshimiwa rais ni zawadi kwa watanzania wote lakini pia ni heshima kwa taifa kutokana na utendaji uliotukuka aliouonesha rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa watanzania.
Mkazi wa Mabogini Japhet Nkya amesema rais Dkt Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi nyingi baada ya kuwaondolea kero ya upatikanaji wa maji katika kata hiyo kero iliyodumu kwa kipindi kirefu na kuwa kama wametengwa.
Amesema pia hata ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya kidato cha kwanza mwakani ni jambo linaloashiria kuwa hakuna mwanafunzi atakayebaki nyumbani kisa ukosefu wa vyumba vya darasa.
0 Comments