Header Ads Widget

RUWASA YAFANIKISHA KUONDOA TATIZO LA MAJI MJI WA KAKONKO

 



Matanki yanayotumika kusambaza maji katika mji wa Kakonko kupitia mradi wa kiziguzigu.

                            xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 SHILINGI Bilioni 5.5 zilizotumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Kiziguzigu wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma umewezesha watu 65,000 kunufaika na huduma ya maji safi na salama yanayosambazwa na Wakala wa maji mjini na Vijijini RUWASA wilaya ya Kakonko  na kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa mji huo.


Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Kakonko, Mhandisi Denis Manji alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajia kunufaisha wananchi katika vijiji 14 katika kata nne za wilaya ya Kakonko na kwamba utekelezaji wa mradi huo kwa sasa umeondoa shida ya maji kwa wakazi wa mji wa Kakonko.


Manji alisema kuwa kwa sasa mradi huo unazalisha lita milioni 1.1 kwa siku ambayo kwa sehemu kubwa yanatosheleza wakazi wa Mji wa Kakonko upatikanaji huo ukifikia asilimia 90 na kwamba kufikia Desemba uzalishaji utaongezeka na kufikia lita milioni 1.8 kwa siku sawa na asilimia 95.


“Kwa sasa uzalishaji unafanyika kwa kutumia vyanzo vinne ambavyo ni visima virefu na kufikia Desemba mwaka huu kisima cha Nyakayenzi kitakamilika na kufanya jumla ya visima vitano kutumika kwa ajili ya usambazaji huo wa maji na kuongeza upatikanaji maji kwa asilimia 95  kwa wakazi wa mji wa Kakonko,”alisema Kaimu Meneja wa RUWASA Kakonko.


Mkuu wa wilaya Kakonko,Kanali Evance Mallasa alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Shirika la maendeleo la Ubelgiji (ENABEL) wamefanya kazi kubwa katika kusaidia kupatikana fedha za kutekeleza mradi wa maji kwa mji wa Kakonko na Vijiji 14 vya wilaya hiyo.


Kanali Mallasa alisema kuwa kwa sasa huduma ya maji safi na salama yanapatikana kwenye vijiji 34 kati ya vijiji 44 vya wilaya hiyo na kwamba serikali kwa bajeti ya mwaka 2022/2023 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.1 ambazo zitatumika kukamilisha  miradi ya maji kwenye vijiji vitano vya wilaya hiyo na shilingi Bilioni 1.1 kuanza ujenzi wa miradi kwenye vijiji vitatu hivyo wilaya kubaki na vijiji viwili ambavyo bado havina miradi ya maji.


“Ifikapo Desemba 2023 wilaya ya Kakonko itakuwa na asilimia 81 ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama na upatikanaji huo utaongezeka na kufikia asilimia ifikapo mwaka 2025, alisema Mkuu huyo wa wilaya Kakonko.


Wananchi wa wilaya Kakonko akiwemo Edina Samwel Mfanyabiashara wa matunda mjini Kakonko alisema kuwa wanaishukuru serikali ya Raisi Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ambapo kwa sasa maji yanapatikana wakati wote karibu na maeneo yao na hawahangaiki tena.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS