Header Ads Widget

RC KATAVI AWATAKA WATUMISHI KUWA WAADILIFU


Watumishi wa Umma Mkoani Katavi wametakiwa kuwa waadilifu wakati wa usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo inakamilika kwa ubora na viwango vinavyotakiwa.


Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Bi.Mwanamvua Hoza Mrindoko  Novemba 10,2022 wakati akikagua Ujenzi wa Vyumba vya Madarasa ya Rais Samia katika Manispaa ya Mpanda ikiwa ni utekelezaji wa ratiba ya kamati ya ulinzi na Usalama Mkoani humo  kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


“Kwa Sasa hivi tunafuatilia ujenzi huu wa madarasa ya Rais Samia ili kuhakikisha kuwa Ujenzi wa Madarasa yanakamilika ndani ya muda uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa.Maelekezo ya Mhe.Rais ni kukamilisha madarasa haya Tarehe 15 Desemba 2022 lakini sisi Mkoa wa Katavi tunasema tutakamilisha Ujenzi huu Tarehe 07 Desemba 2022 ili ile wiki moja iwe ni ya Waziri wa TAMISEMI kufanya ufuatiliaji  na kumkabidhi Mhe.Rais.”Alisema Mkuu wa Mkoa Mrindoko.


 Bi.Mrindoko  ameipongeza Manispaa ya Mpanda kwa kusimamia vizuri Ujenzi wa madarasa ya Mhe.Rais Samia ambapo amewataka kuongeza jitihada zaidi ili kuhakikisha kuwa Ujenzi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.


“Nyie Manispaa ya Mpanda mnaongoza kwa kuwa na vyumba vingi vya madarasa na mna vyumba 51 kati ya 119 na katika maeneo niliyopitia nimeridhishwa na hatua nzuri ya ujenzi hivyo msibweteke na sifa na badala yake mjipange kuhakikisha kuwa mnakamilisha Ujenzi ndani ya muda uliopangwa”alisema Bi.Mrindoko.


Aidha Bi Mrindoko ametoa rai kwa Wananchi kuendelea kuchangia nguvu kazi katika Ujenzi wa Madarasa 119 ili Shilingi Milioni Ishirini iliyotolewa kwa kila darasa itosheleze kumaliza ujenzi huo ambapo amewataka Wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa kia darasa ndani kunakuwepo na viti na meza kwa ajili ya Wanafunzi.


Akiwa Manipaa ya Mpanda Mkuu wa Mkoa Bi Mwanamvua Mrindoko amekagua Ujenzi wa Vyumba vya madarasa katika Shule za Sekondari Lyamba,Rungwa,Shanwe,pamoja na Mpanda.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS