MKOA wa Pwani umeendelea na mikakati ya kuhakikisha wafanyabiashara na wenye viwanda wanazalisha bidhaa bora na zenye viwango.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda Uwekezaji na Biashara mkoa wa Pwani Rehema Akida wakati wa kufungua mafunzo ya utumiaji mifumo ya biashara yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Akida amesema kuwa watahakikisha wanatumia taasisi mbalimbali zinazotoa mafunzo ya namna ya uboreshaji bidhaa ili ziingie kwenye ushindani wa soko na mataifa mengine.
"Bidhaa zao zikiwa bora wataboresha uchumi wao wa mkoa na Taifa kwa ujumla na pia wajitangaze kwa kushiriki kwenye maonyesho na mafunzo mbalimbali," amesema Akida.
Amesema kuwa wataboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kushirikisha taasisi mbalimbali ili ziwaongezee ujuzi na maarifa ili kushindana na wengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Biashara toka Tantrade Twilumba Mlelwa amesema kuwa mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wazalishaji wenye viwanda ili watambue Masoko.
Mlelwa amesema kuwa malengo mengine ni kuhakikisha wanapata Masoko endelevu na kufuata taratibu mbalimbali wanazopaswa kuzifuata hasa pale wanapotaka kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa kutumia taasisi zikiwemo TRA, TBA na BRELA ili wasipate vikwazo.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka amesema kuwa wanaomba taasisi mbalimbali kujitokeza kuwasaidia ili waweze kuboresha bidhaa zao ikiwa ni kupata mafunzo kama hayo ambapo bidhaa zikiuzika uchumi utakuwa na ajira zitaongezeka na serikali itapata mapato pia itavutia wawekezaji toka nje.
0 Comments