Adeladius Makwega-MBAGALA
Kijana huyu amefanya kazi mbalimbali,
kwa maoni yangu nina hakika katika kila nafasi aliyowahi kupewa amezitendea
haki, japokuwa anakutana na changamoto nyingi. Kwa maoni yangu ya hakika pahala
ambapo kuna misuguano mingi ndipo maendeleo ya wengi yanaweza kupatikana.
Sehemu isiyo na misuguano moto hauwezi kuwaka na mara zote watu watakula
chakula kibichi.
Katika ulimwengu wa leo, Je
yupo anayependa kula chakula kibichi ? Mwanakwetu hapana ndilo jibu lake. Misuguano
lazima iwepo kwa manufaa ya wengi.
Kwa bahati nzuri kijana huyu
mahiri niliyekutana naye binafsi namfahamu sana tangu akiwa mwanafunzi wa Shule
ya Msingi Bunge, huku mimi nilikuwa nikidoea kusoma hapo kwa kufanya mitihani
ya majaribio kila jumamosi, kwa hisani baba yangu ambaye alikuwa mwalimu wa
shule hii kongwe ya umma.
Shule hii aliyosoma kiongozi
huyu tangu enzi ilikuwa na wanafunzi wengi ambao baba/ mama zao wakiwa viongozi
serikalini na kwa wakati huo kupata nafasi ya kuingia darasa la kwanza ilikuwa
kazi kidogo. Ndugu yangu huyu tangu wakati huo hulka yake ya ukweli, ya kueleza
jambo wazi wazi alikuwa nayo. Binafsi sikuwa jirani naye, kwani kazi yangu
ilikuwa ni kwenda kufanya mitihani hiyo na kuondoka zangu, mitihani yangu niliyoifanya
nilikuwa napewa jumamosi inayofuata kwa hisani ya baba.
Shule hii aliyosoma ndugu
yangu huyu ilikuwa na watoto wengi wa viongozi wakiwamo hata watoto wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo Ali Hassan Mwinyi, sitaki kujadili tabia
zao, hulka zao na hata majina ya watoto hao wa viongozi waliosoma wakati huo maana
leo hilo siyo ajenda yangu, lakini huyu jamaa alisoma nao. Binafsi sifahamu
ndugu huyu aliwezaje kusoma shuleni hapo? Nadhani alipokuwa analelewa wakati
huo Jijini Dar es Salam palikuwa nyumbani pa mkubwa.(Sitaki kuingia ndani
katika hili kwa kuwa siyo ajenda yangu ya leo.)
Kumbuka msomaji wangu nipo
katikati ya Jiji la Dar es Salaam, niko na ndugu yangu huyu, sasa akaniuliza
habari za mwalimu wake, nikamjibu hajambo na kumpatia nambari yake ya simu.
Akampigia simu lakini mwalimu hakupokea simu hiyo na hilo likatupa nafasi
tukaendelea na mazungumzo yetu.
Nikaulizwa Mwanakwetu mbona
katikati ya jiji leo hii kulikoni ? Una biashara hapa Posta? Nikamjibu nitoe
wapi kaka! Nikasema hapa kuna kazi moja naifanya, nikualike ushiriki? Akacheka
sana, alafu akasema kaka unanitakia mema? Akasema,
“Mwanakwetu haya mambo unayajua
vizuri sana tangu tunasoma. Unakumbuka mwalimu hasahihishi madaftari yetu hadi
visheti vyake vyote vinunuliwe? Mapumziko utanunua ice cream, maandazi na
mihogo lakini pesa ya kisheti cha mwalimu lazima uiweke ili daftari lako
lisahihishwe vizuri. Vinginevyo wewe kila siku daftari lako halitosahihishwa
kamwe. Nikionekana katika sherehe watasema jamaa kaacha kituo cha kazi, sasa
yupo katika sherehe tu, si mnamuona? Kama yale yale ya mwalimu muuza visheti.
Wanafunzi kuepusha maneno unakuwa na pesa ya kununua visheti vya mwalimu”
Nikacheka sana nikauliza Je
visheti vya vimechomwa vizuri? Je vina sukari ya kutosha? Je vimeiva? Jamaa
akajibu, “Mwanakwetu jukumu lako ni kuvinunua tu ili mwalimu akusahihishie
daftari lako, ukivila au ukivigawa shauri ni lako. Unapokuwa na damu ya
kunguni, mwanakwetu ishi kwa tahadhari.”
Nikamwambie hilo kweli kabisa,
maana mwenye godoro akilala akishaumwa na kunguni na mwili wake kuanza
kumuwasha asubuhi lazima aanze kuwasaka kunguni hao mmoja baada ya mwingine.
Kama ataanika juani, atapiga dawa, atatumia maji moto kubwa ni kuwasaka kunguni
tu katika godoro / kitanda /nguo zake.
Wakati mwingine unaweza
ukatokea moto ukamuunguza mwenye godoro, godoro lenyewe na kunguni, hii ni
hasara kwa wote. Lakini mwenye godoro anaweza kufariki watu wanagawana urithi
wa vitu vya marehemu–magodoro/vitanda /nguo na samani zote. Kumbe hapo mnapogawana
na wengine wanarithi kunguni. Hapo mwanakwetu inakuwa bahati ya kunguni kupata
makazi mapya.
“Mungu kaumba viumbe vyake
kaka, hata kunguni na wao wamo na ndiyo maana kuna bahati ya kunguni kama hii.” Ndugu yangu huyu akacheka sana.
Wakati wewe unasema una damu
ya kunguni kumbuka pia kuwa kuna bahati ya kunguni ya kuwepo katika mgao wa
samani za marehemu, ndugu huyu alikuwa anacheka zaidi
Kweli ndugu yangu huyu alipomaliza
mazungumzo haya alituaga na kwenda zake kurudi kituo chake cha kazi na mimi
kubaki hapo nikikamilisha majukumu yangu, kubwa nilimkumbuka mwalimu wangu
mmoja wa Kichaga aliyekuwa anauza visheti shuleni Mnazi Mmoja wakati huo na
hasahihishi madafatari hadi visheti
vyake viishe.
0 Comments