Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wananchi wa kijiji cha Nyombo wilayani Njombe wameiomba serikali kukamilisha kwa haraka utekelezaji wa mradi wa maji utakaowahudumia takribani wakazi 4144 ili waweze kuondokana na changamoto ya kutumia maji machafu ya mito na visima yanayowasababishia homa ya matumbo na kuhara mara kwa mara.
Mradi huo uliotajwa kufikia asilimia 75 katika utekelezaji wake utakwenda kupunguza changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji ambapo baadhi ya wananchi wa kijiji hicho akiwemo Anastazia Mbata na Ezekia Mligula wamesema wameendelea kutaabika kwa miaka mingi kukosa maji safi na salama hivyo mradi unaoendelea kutekelezwa endapo utakamilika utawasaidia sana kupunguza changamoto hizo pamoja na kumtua mama ndoo.
Meneja wa wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Njombe mhandisi Elikalia Malisa amesema kikwazo cha ukamilishaji mradi huo utakaogharimu zaidi ya shilingi milioni 800 kilikuwa ni changamoto ya hali ya hewa wakati wa kuanza kuutekeleza pamoja na malipo kwa mkandarasi licha ya maendeleo mazuri yaliyopo.
Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Mhandisi Msafiri Mtyauli ameomba kupatiwa kwa fedha anazodai ili aweze kutekeleza mradi huo kwa haraka kwani asilimia kubwa amefanyakazi hiyo pasina malipo.
Mkurugenzi mkuu wa wakala wa maji vijijini RUWASA nchini Mhandisi Clement Kivegalo amefika kijijini hapo kushuhudia utekelezaji wa mradi huo ambapo amekiri kuwa serikali itakwenda kumlipa fedha hizo na kumtaka kwenda kukamilisha kazi hiyo haraka iwezekanavyo na ifikapo disemba 25 wakati wa krismas wananchi wawe wanapata maji safi ya bomba.
Hadi sasa ujenzi wa vituo vya kuchotea maji katika mradi huo umefikia asilimia 90 hivyo pindi mkarndarasi atakapokamilisha kazi zake maji yataanza kutoka.
0 Comments