Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imewaachia huru
makada wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Katala Kikaja na
Ng'hulima Lilanga waliohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya wizi,
unyang'anyi wa kutumia silaha na ubakaji.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Novemba 16, 2022 na
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Athuman Matuma baada
ya kuridhika na hoja za warufani kuwa ushahidi uliowatia hatiani Aprili 12,
mwaka huu, ulikuwa dhaifu, unaotia mashaka na usiokubalika mbele ya macho ya
sheria.
Wana Chadema walitiwa hatiani kwa makosa mawili ya wizi,
ubakaji, kuharibu mali na unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya kukamatwa
wakiwa kituo cha kupigia kura Kata ya Dutwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu
walikokuwa mawakala wa wagombea wa chama hicho kikuu cha upinzani katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.
Pamoja na wizi wa Sh300, 000 warufani hao kwa pamoja
walidaiwa kumbaka msaidizi wa kituo cha kupigia kura ambaye jina lake
lilihifadhiwa kulinda utu na heshima yake mbele ya jamii.
Tangu walipokamatwa siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28,
2020, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo Aprili 12, mwaka huu,
warufani hao wamekaa mahabusu na gerezani kwa takribani miaka miwili na miezi
mitatu kutokana na shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha ambayo ni moja ya
mashtaka yaliyokuwa yanawakabili kutokuwa na dhamana.
Hadi kuachiwa huru leo, warufani hao wametumikia takribani
miezi saba ya adhabu yao katika magereza ya Bariadi, Shinyanga na Butimba
jijini Mwanza.
0 Comments