Bweni la wanafunzi wa kike shule ya Kakonko Girls wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma
Mkuu wa wilaya Kakonko Kanali Evance Mallasa
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
HALMASHAURI ya wilaya Kakonko mkoani Kigoma imeanza kutekeleza mpango mkakati wa halmashauri hiyo wa kuinua elimu ya juu kwa wasichana ikiwemo masomo ya sayansi ili kuhakikisha wanafunzi wengi wa kike wanaendelea na elimu ya juu ya vyuo vikuu.
Kaimu Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Michael Faraay akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa alisema kuwa moja ya utekelezaji wa mpango huo ni ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ambayo itakuwa na mahitaji maalum kwa ajili ya kutimiza mahitaji ya kupata elimu kwa wasichana hao.
Faraay alisema kuwa tayari shule ya sekondari ya wasichana Kibondo imeshaanza kwa mwaka huu kuchukua wanafunzi 82 wa kidato cha kwanza ambao wanakaa bweni na mpango huo umeanza kuzaa matunda kwani wanafunzi wote tangu mwezi januari hadi sasa wanaendelea vizuri na masomo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa shule hiyo ambayo ina michepuo ya masomo ya sayansi imewekwa kwenye mpango maalum kuhakikisha wanafunzi wasichana wanasoma vizuri na kufaulu kwa wastani wa juu kwenye masomo ya sayansi mpango ambao utawawezesha kuendelea na masomo ya vyuo vikuu kwa kozi zinazotokana na masomo hayo.
Kwa upande wake Afisa elimu Sekondari wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Christopher Bukombe alisema kuwa wilaya imepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 760 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 38 vya sekondari kwenye wilaya hiyo lakini vyumba vinane vimepelekwa shule ya sekondari ya wasichana Kakonko.
Alisema kuwa mpango huo unakuja kuondoa changamoto ya idadi kubwa ya wasichana kushindwa kumaliza elimu ya sekondari ambayo imekuwa ikiwakumba ikiwemo umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shule, suala la mimba na wengine kutokuwa na ari ya kusoma na kuamua kuolewa.
Sambamba na hilo pia wanaendelea na mpango wa ujenzi wa bweni kwenye shule ya Sekondari ya Kakonko ili kuongeza idadi ya wanafunzi wasichana wanaokaa bweni waweze kuondokana na changamoto zinazokwamisha mipango yao ya kitaaluma.
Mkuu wa wilaya Kakonko, Kanali Evance Mallasa alisema kuwa ujenzi wa madarasa 38 yenye thamani ya shilingi 760 ni jambo kubwa kwa wilaya hiyo ambalo limefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa madarasa kwa wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwakani.
Kanali Mallasa alisema kuwa pamoja na hilo wilaya imeendelea kutekeleza mpango wake wa kutafuta rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wasichana ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali na kushindwa kumaliza masomo kwa idadi kubwa.
0 Comments