Na Matukio daima media, Chunya
Wananchi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wametakiwa kuwasaidia watoto yatima,wajane na wahitaji ili waweze kuwapa faraja na wao kupata thawabu mbele za Mungu.
Wito huo umetolewa na Shamim Ayoub Omary mfanyabiashara maarufu wilayani Chunya katika hafla ya matendo ya huruma(Udiakonia)iliyoandaliwa na Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Chunya Mjini.
Shamim amesema ni vema jamii ikajiwekea malengo kwa kutenga sehemu ya kipato kwa ajili ya kusaidia jamii wakiwemo yatima,wajane na watu wanaoshi mazingira magumu.
"Mimi na mume wangu Ayoub Omary tumekuwa tulitenga sehemu ya kipato chetu kwa ajili ya wahitaji na jamii kwa ujumla"alisema Shamim.
Kupitia sadaka hiyo tumekuwa tukimuona Mungu na baraka nyingi zimekuwa zikimiminika katika familia yetu.
Aidha katika hafla hiyo mbali ya kukabidhi misaada mbalimbali kwa wahitaji alikabidhi fedha taslimu shilingi laki mbili kwa ajili ya kuchangia mfuko wa Udiakonia.
Mchungaji Robert Sikanyika wa Ushirika wa Chunya Mjini amemshukuru mfanyabiashara huyo kwa misaada mbalimbali anayoitoa kwenye jamii.
Sikanyika amesema hafla ya mwaka huu imepata mwitikio mkubwa kwenye Kanisa na jamii kwa ujumla bila kujali madhehebu wameweza kukusanya fedha,nguo,viatu,vyakula na mahitaji kwa watoto wa shule.
Mchungaji Sikanyika amesema kama Kanisa zoezi hilo ni endelevu na kila mwaka wamekuwa wakiyahudumia makundi hayo.
Naye Mwenyekiti wa Udiakonia Ushirika wa Chunya Mjini Robson Kalua amesema mwaka huu wamewagusa wahitaji zaidi ya mia mbili wakiwemo wazee,watoto na watu wenye ulemavu.
Amesema mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la wahitaji hasa kutokana na zoezi hilo kuhusisha ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia Ustawi wa jamii ambao walisaidia kuzibaini kaya zenye uhitaji.
Amewapongeza waumini na wadau wengine nje ya Kanisa ambao wametoa msaada wa hali na mali ambao wengi wao wametoa vitu vipya kutoka katika maduka yao.
Baadhi ya wanufaika wamesema msaada walioupata umewapa faraja kubwa na kujiona nao wanathamani kwenye jamii.
0 Comments