Header Ads Widget

WANANCHI WAAMBIWA TUNZENI NA KULINDA MIRADI YA MAJI-DC NZEGA


Mkuu wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora ,Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP),Advera Bulimba akizungumza na wananchi wa  kijiji cha wita juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji

Mratibu wa Shirika la World Vision wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala AP, Michael Ngasa alimweleza jambo Mkuu wa Wilaya ya Nzega aliyevaa suti nyeusi na katikati ni Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega, Jacqueline Kaihura

                xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Lucas Raphael,Tabora

 Mkuu wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora ,Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP),Advera Bulimba amewataka wananchi kutunza na kulinda miundombinu na miradi ya  maji iliyoko kwenye maeneo yao ili iweze kuwahudumia kupata maji safi na salama uliogharimu  shilingi milioni 464,557,269.55.

 

Hayo yalisemwa jana katika hafla fupi ya kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa mradi wa maji iliyofanyika  katika kijiji cha Wita Kata ya Ndala wilayani humo  .

 

 Bulimba alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika wilaya hiyo wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji hivyo ni jukumu la wananchi kulinda na kuitunza miradi hiyo kwa manufaa yao.

 

Alisema mradi huo wa maji umejengwa kwa ushirikiano kati ya serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Nzega pamoja na Shirika la World Vision Tanzania kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala-AP wilayani humo.

 

 Alisema kuwa Wadau wakubwa na muhimu katika kulinda na kutunza  mradi huo pamoja chanzo cha maji ni watumiaji maji pamoja na wananchi waishio katika maeneo jirani na chanzo hicho hivyo ni muhimu wakavilinda kwa uangalifu bila kuviharibu.

 

 "Wadau wakubwa na ambao ni muhimu katika utunzaji wa vyanzo vya maji ni watumiaji maji na wananchi wanaoishi katika maeneo jirani vilipo vyanzo vya maji  hivyo ni muhimu kuelimishwa kuhusu kutumia maji kwa  busara,uangalifu na kwa tija bila kuharibu chanzo wala miundombinu ya maji "amesema.

 

 Alisema kuwa utunzaji wa mradi huo na chanzo cha maji ambacho ni kisima kirefu kilichoko katika kijiji hicho  ni suala mtambuka ambalo linawahusisha wadau mbalimbali na wananchi wakiwemo na kuhakikisha watu wote watakaohusika kuhujumu mradi huo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

 

 Bulimba aliendelea kueleza kuwa  suala la kuhifadhi vyanzo vya maji limekuwa likitiliwa mkazo na serikali ya awamu ya sita ya inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ili afikie adhima yake ya kumtua mama ndoo kichwani ifikapo mwaka 2025.

 

 Aidha alilitaka jeshi la jadi la Sungusungu katika kijiji hicho kuhakikisha mradi huo unalindwa kwa nguvu zote na kuwadhibiti watu wote wenye nia ovu ya kuhujumu mradi huo muhimu kwa wananchi wa kijiji hicho.

 

 Naye Mratibu wa Shirika la World Vision wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala AP, Michael Ngasa alimweleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa kwa kushirikiana na Ruwasa wameweza kuhakikisha mradi huo unakamilika na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

 

 Alisema kuwa mradi huo wenye vituo vya kuchotea maji 12 unawahudumia jumla ya wananchi 3401 katika kijiji hicho na umegharimu jumla ya Sh 464,557,269.55 huku Shirika hilo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala  likitoa kiasi cha Shilingi milioni  297,827,869.55 katika fedha hizo.

 

 "Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na mambo mengine ya utekelezaji wa miradi yetu moja ya shughuli kubwa tuliyofanya ni kuhakikisha tunashirikiana na Ruwasa kukamilisha mradi huu wa maji wa Wita,"amesema.

 

 Awali Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nzega,Mhandisi Faustine Makoka alisema kuwa kwa sasa mradi huo umekamilika na umeanza kutumika na changamoto iliyopo kwa sasa ni wananchi kushindwa kuunganisha maji majumbani kutokana na gharama kubwa za maunganisho.

 

 "Huu mradi umekamilika ni mradi mkubwa na sasa wananchi walio wengi wanapata maji kupitia vituo vya kuchotea maji na changamoto ambayo tunayo ni wananchi kushindwa kuunganisha maji majumbani kutokana na gharama kubwa,"amesema.

 

 Mhandisi Makoka alisema ili kumaliza changamoto hiyo ofisi ya Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nzega itatoa mabomba pamoja na dira za maji kwa Jumuiya ya Kamawinu ambao ndiyo wanasimamia mradi huo ili iweze kuwaunganishia wananchi maji majumbani kwa bei nafuu ambapo gharama zitapungua kwa kiasi kikubwa sana.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS