NA TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera.
MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewaasa wananchi mkoani humo kuandaa chakula cha kutosha kitakachoweza kulisha wageni ambao wamekuja katika kuadhimisha kilele cha Mwenge wa Uhuru.
Chalamila ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari katika Uwanja wa Kaitamba Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera baada ya kumaliza kukagua maandalizi ya sherehe hizo ambapo amesema kuwa ame pokea malalamiko kutoka kwa wageni ambao wamewasili mkoani humo juu ya kuwapo changamoto kwa baadhi ya huduma za chakula.
“Tumeishaanza kupokea wageni katika mkoa wetu ambao wanakuja katika maadhimisho ya kilele cha Mwenge wa Uhuru yatakayofanyikia mkoani hapa katika Uwanja wa Kaitaba ila baadhi ya wageni wameanza kuwasilisha malalamiko ya uwepo wa changamoto katika baadhi ya huduma, mfano huduma ya chakula, hivyo nitoe rai kwa wananchi wa Kagera andaeni vyakula vya kutosha kwani ugeni huu ni mkubwa mno” alisema RC Chalamila.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzimwa Oktoba 14 mwaka huu mkoani Kagera tayari umezungukia wilaya zote za mkoa huo na kuweza kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku hiyo ya kihistoria.
“Mwenge wa Uhuru umemulika miradi 37 yenye jumla ya Shilingi Bil.13.6 katika mkoa wetu na miradi hiyo yote inakaguliwa na inatembelewa ili kuangalia kama ina kasoro ya aina yoyote, tumepewa heshima kubwa na Rais wetu ya kufika katika mkoa wetu Oktoba 13 mwaka huu.
Rais atafanya kazi ya kupokea na kuzindua Chuo cha VETA pale Mgeza Bukoba Vijijini”alisema Chalamila.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Sera na Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amewataka Watanzania kuendelea kuenzi Mwenge wa Uhuru kwani ni chanzo cha umoja na mshikamano nchini.
“Mwenge huu unapita mikoa yote ya Tanzania, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa ndiyo wanakuwa wakipokezana mwenge huo, kuna watu wengine wamekuwa wakifikiria kuwa mwenge huu unatembea tu ila wanatakiwa kujua umoja na mshikamano wetu tulionao ya kuwepo nchini moja ya sababu kuu ni Mwenge wa Uhuru”alisisitiza.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako wa wakati akikagua maandalizi ya sherehe hizo amesema yamefikia hatua nzuri ambap amesema kila kitu kipo sawa ukiwamo ulinzi huku akiwaomba wananchi wa Mkoa wa Kagera kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwani mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwisho
0 Comments