Header Ads Widget

WANAFUNZI KIDATO CHA 4 WATAKIWA KUMTANGULIZA MUNGU MBELE KWENYE MITIHANI YAO

 



WANAFUNZI wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne hivi karibuni wametakiwa kumtanguliza Mungu ili awezeshe kufanya vizuri mitihani yao.


Hayo yalisemwa Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro na Profesa Jumanne Maghembe  wakati wa mahafali ya nane ya kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Vuchama.


Maghembe alisema kuwa  Mungu anamsaidia anayesoma na kutenda na Mungu atawabariki na kuwajalia kama watamwomba hata wakitaka kuwa madaktari au wanasheria watafanikiwa.


Alisema kuwa pia waweke malengo ndiyo yatakayowafanya wanafunzi waweze kufanikiwa katika masomo yao kwani malengo hayo ndiyo maisha yao.


"Wasiokuwa na malengo wanakuwa wanapoteza muda wao hivyo bila lengo utawaacha wenzako wenye malengo wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kuja kuwa na kazi na maisha mazuri huku wale wasio na malengo wakipata kazi ndogo ndogo zisizo na hadhi,"alisema Maghembe. 


Meneja wa shule hiyo Yasin Mfinanga alisema kuwa watapambana kwa hali na mali kuhakikisha shule inafanya vizuri na kutaka wasome hadi wawe ma Profesa ili waweze kuja kulisaidia Taifa kupitia elimu waliyoipata ambapo safari yao bado inaendelea.


Kwa upande wake Mkuu wa Shule Jumanne Mkoga alisema kuwa mwaka huu wanataka kufanya vizuri kwenye mtihani wa Taifa kwa kushika namba 10 bora kwani kuna baadhi masomo wamekuwa wa kwanza kimkoa masomo hayo ni jografia, kemia na baiolojia hivyo uhakika wa kushika nafasi hiyo na wamejipanga vizuri kwa kuwaandaa vizuri kitaaluma.


Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Leila Msuya alisema kuwa shule yao imepata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuongeza ufaulu kuboresha maktaba kununua vitabu na kuhifadhi mitihani ya miaka iliyopita na kununua vifaa vya maabara na kuwa na mtaalamu kuongeza jengo la kompyuta na kompyuta.


Moja ya wazazi Kawanga Itendo alisema kuwa wanaridhishwa na elimu watoto wao wanayopewa shuleni hapo kuanzia elimu ya kawaida na elimu ya dini na wao kama wazazi watahakikisha wanawapa mahitaji yote watoto wao ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao ili wawe hazina ya baadaye ya Taifa. Jumla ya wahitimu 45 walipewa vyeti vya kuhitimu kidato cha nne.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI