Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa uwelewa mdogo wa wananchi juu ya ulipaji wa kodi ya ardhi pamoja na huduma za kibenki kutokufika vijijini ni miongoni mwa changamoto zinazopelekea Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kutofikia malengo ya kufikia ya ukusanyaji kodi iliyojiwekea.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati alipokutana na wadau wa ukusanyaji maduhuli ili kujadili jinsi ya kutoa elimu kwa wananchi na kuongeza ukusanyaji wa mapato lengo ikiwa ni kutekeleza agizo la Serikali la ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletroniki.
Amesema kuwa, bado maeneo ya vijijini huduma za kibenki hazijawafikia wananchi wengi hivyo kupelekea wizara hiyo kutofikia lengo la ukusanyaji wa mapato pamoja na uelewa mdogo kwa wananchi katika kufanya miamala.
"Kupitia kodi ya Ardhi tumelenga kusanya bilioni 200 kwa kipindi cha mwaka 2021/22 ila tumefanikiwa kukusanya kodi kwa asilimia 60 tu na hii inatokana na changamoto za uelewa mdogo wa kufanya miamala hususani vijijini pamoja na wengi wao kuona usumbufu kufunga safari kwenda mjini kwa lengo la kulipa kodi"amesema Dkt. Kijazi.
Aidha amewaomba wadau wa kampuni za simu na benki kushirikiana na wizara katika utoaji elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi na jinsi ya kulipa kupitia njia ya benki na simu kwani itaisaidia serikali kuongeza mapato na wao kufaidika kupitia ulipaji huo wa kodi.
"Benki nyingi zina mifumo ya kuelimisha wananchi kwa njia ya kidijitali, sambamba na kampuni za simu hivyo tunaziomba kutumia njia hizo pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji maduhuli na jinsi ya kufanya miamala ili kukusanya Mapato ya Serikali kwa kiwango stahiki" Ameongeza Dkt Kijazi .
Hatahivyo amesema kuwa kupitia kampuni za simu wataweza kuwafikia wananchi wa vijijini na kuwarahisishia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kulipa kodi hiyo kwenye benki.






0 Comments