***********
Na Amon Mtega, Mbinga.
MWENYEKITI Mpya wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Mdaka amewataka wanachama wa Chama hicho hasa Viongozi kuzingatia taratibu na kanuni ikiwemo kuvaa sale za chama wakati wa vikao.
Wito huo ameutoa wakati akiongoza kikao cha Halmashauri kuu ya Wilaya hiyo ambacho kilikuwa maalumu kwaajili ya kuwachagua Wajumbe watatu wa kamati ya siasa huku kikiwa kimehudhuliwa na wabunge wa majimbo yote mawili Mbinga Vijijini Benaya Kapinga na Mbinga mjini Jonas Mbunda.
Mdaka ambaye pia amewapatia katiba mpya za CCM 48 kwa kila kata katiba moja na kata zipo 48 ili zikawasaidie kutafsiri sheria na kanuni za chama amesema kuwa haiwezekani kiongozi anakuja kwenye kikao kikubwa kama hicho bila kuvaa sale jambo ambalo halitakiwi kwa kuwa litakuwa linarudisha nyuma uhai wa Chama.
Aidha mwenyekiti huyo akitangaza matokeo ya uchaguzi wa kuwapata Wajumbe watatu wa kamati ya siasa kuwa ni James Mapunda ambaye ameongoza kwa kura 161 ,wapili Gervas Nchimbi kura 139 na Mariether Mponda amepata kura 118 (Mama Madaba)na ambao kura hazijatosha kutoka kwa Wajumbe ni Victoria Milinga kura 73 , Andrew Matambi kura 44 na Daniel Chindengwike kura 35.
Kwa upande wake James Mapunda ambaye ameongoza kwa kura amewashukuru Wajumbe hao kwa kumuamini kumpa kura za kishindo ameahidi kuwatumikia kwa kushirikiana na Viongozi wenzake.
Naye katibu wa CCM Wilaya ya Mbinga ambaye naye ni mpya Mary Mwenisongole wakati akijatambulisha kwa mara ya kwanza kwa Wajumbe wa mkutano huo amesema kuwa amekuja kuendelea kukiimarisha Chama pamoja na kusimamia utekelezaji wa Ilani inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwisho.
0 Comments