CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba Serikali kupandisha kiwango cha mishahara kwa watumishi wa kada ya Elimu ili kuendana na hali ngumu ya maisha ya sasa
Hayo yamebainishwa na kaimu Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Dinah Mathamani katika kikao cha majumuisho ya Ziara iliyofanywa na viongozi hao wa ngazi ya Taifa Mikoa na wilaya kutoka katika kanda ya Kusini na Mashariki ya kutembelea Shule mbali mbali za Mkoa wa Lindi sambamba na kuzungumza na walimu .
Mikoa hiyo iliyokutana ni pamoja na Mkoa wa Morogoro, Dar es salam, Pwani , Ruvuma, Mtwara na wenyeji Lindi.
Mathamani alisema pamoja na kushukuru jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Rais Samia za kuboresha Makazi ya Walimu lakini bado mishahara wanayopokea hailingani na gharama za maisha kwa wakati uliopo hivi sasa .
" tunatambua kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/2023 imetenga shilingi milioni 55 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 859 za walimu ambazo zitaenda kuboresha makazi ya walimu wetu"
"Lakini kulingana na jinsi ambavyo gharama za maisha zilivyo hivi sasa mafuta yamepanda, bei ya vyakula imepanda bado mishahara wanayopokea walimu wetu haitoshelezi mahitaji tunajua Rais wetu ni msikivu sana atatuongeza mishahara kwa maka ujao" alieleza
Hata hivyo aliomba Serikali kurudisha posho ya kufundishia kwa walimu kama ilivyo kwa miaka ya nyuma ili kufanya mazingira ya kufundishia kuwa kwa walimu kuwa mepesi.
"Tunasema kazi ya kawaida ni masaa nane lakini Mwalimu anafanya kazi zaidi ya masaa nane , anamaliza kufundisha kwa masaa hayo lakini bado kusahihisha, kuandaa masomo, kuangalia mitihani kuandaa zana za kufundishia na kadharika ndio maana tunasema posho kwa ajili ya walimu Serikali haiwezi kukwepa " alifafanua Mathamani.
Kwa upande wake kaimu katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania mwalimu Japhet Maganga alisema kuwa Katika kuhakikisha huduma za wanachama wao zinaboreka pesa zinazopatikana zinaendelea kurudi kwa wanachama wao .
Alisema hiyo itasaidia kuwafanya viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa kuwatembelea walimu ambao ni wanachama wao kuzungumza ili kubaini changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitatua.
Nae mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Lindi Mwalimu Alima Liveta alisema kuwa viongozi hao wa chama cha walimu zaidi ya mia tatu waliofika katika mkoa huo wa Lindi kutoka katika kanda ya kusini na Mashariki wameweza kutembelea katika Shule mbali mbali za mkoa huo na kuzungumza na walimu ambapo pamoja na mambo mengine lengo likiwa ni kutangaza chama hiko cha Walimu.
Alisema viongozi hao pia walipata fulsa ya kuzungumza na walimu kutangaza Benki yao ya Walimu, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji kazi baina ya Mikoa hiyo , kutambua Changamoto wanazokabiliana nazo walimu kwa lengo la kuinua taaluma kwa ngazi ya mikoa na Taifa kwa ujumla.
0 Comments