Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, Mhandisi Athanasius Nangali na Kushoto kwake ni Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Singida Mhe. Jesca Kishoa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Matengenezo wa Kituo hicho cha Kufua Umeme cha Kinyerezi II Mha. Benjamin Mghuna, namna Mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na Mvuke inavyofanya kazi, wakati kamati hiyo ilipokitembelea kituo hicho Oktoba 13, 2022.Kushoto kwake ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kamishna Msaidizi wa Masuala ya Gesi, Mhandisi Fakihi Mohamed na anayefuatia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania Mhandisi Athanasius Nangali.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiwa katika picha ya pamoja wakati Kamati hiyo ilipotembelea kituo hicho Oktoba 13, 2022.
Kituo cha Kufua Umeme cha Kinyerezi II, kinachozalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na Mvuke chenye uwezo wa kuzalisha 240 MW kinavyoonekana pichani.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Dorina G. Makaya- Dar-es-Salaam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeupongeza Uongozi wa TANESCO na Watumishi wa Kituo cha Kufua Umeme cha Kinyerezi II kinachozalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na Mvuke, kwa kudumisha usafi, kuendesha mitambo na kuikarabati kwa weledi pamoja na kuwa na mikataba ya muda mrefu ya upatikanaji wa vipuri kutoka kwa waunda Mitambo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dunstan Kitandula, baada ya Kamati hiyo kutembelea Kituo hicho cha Kufua Umeme cha Kinyerezi II, kinachozalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na Mvuke chenye uwezo wa kuzalisha 240 MW na kupata maelezo kutoka kwa Uongozi wa TANESCO na wa Kituo hicho Oktoba 13, 2022.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ameutaka Uongozi wa TANESCO kuongeza chanzo cha maji kwa ajili kutumika katika kuzalisha umeme kwa kuchimba kisima cha maji ambacho kinaweza pia kutumiwa na DAWASA katika muda ambao kisima hicho hakitumiki na Kituo cha Kinyerezi II.
Aidha, Mhe. Kitandula, ameikumbushia TANESCO kuwa, kwa vile inajua muda wa matumizi ya mitambo iliyofungwa, ihakikishe inajiandaa kuweka mitambo mipya pindi mitambo iliyopo itakapokwisha muda wake.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kamishna Msaidizi wa Masuala ya Gesi, Mhandisi Fakihi Mohamed, ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea Kituo hicho na kuwapatia maoni mazuri na ya kimkakati na kuahidi kuwa maoni hayo yatazingatiwa katika maandalizi na maboresho ya mikakati ya Wizara katika kuongeza kasi ya utendaji na ufanisi katika Sekta ya Nishati.
Vilevile, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, Mhandisi Athanasius Nangali, ameishukuru kamati hiyo kwa kutembelea kituo hicho na kuahidi kutekeleza maoni na mapendekezo ya Kamati hiyo ipasavyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya Bunge kituoni hapo, Mkuu wa Matengenezo wa Kituo hicho cha Kufua Umeme cha Kinyerezi II Mhandisi Benjamin Mghuna, aliielezea kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini namna Mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia na Mvuke inavyofanya kazi.
Kamati hiyo ilitembelea kituo hicho na kujionea sehemu mbalimbali muhimu Pamoja na Mitambo inayotumika kuzalisha umeme Kituoni hapo.
0 Comments