Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu amepokea vikombe ambayo wizara hiyo imepata ushindi katika mashindano ya Shirikisho la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2022 yaliyofanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga.
Mapokezi hayo yamefanyika jana Oktoba 21, 2022 Mtumba jijini Dodoma ambapo timu ya wizara hiyo ni miongoni mwa timu ambazo zimeshiriki vema mashindano ya SHIMIWI na kuwa miongoni mwa timu zilizopata vikombe na medali katika mashindano hayo.
Akipokea vikombe viwili na medali mbili ambazo wizara hiyo imepata Kaimu Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema “Inafurahisha sana tukiwa tunazungumza hivi na vikombe tunavitazama, hili jambo ni jema na linafurahisha sana, spiriti hapa michezo ni upendo, furaha, Amani, kufahamiana na kujenga afya”.
Vikombe ambavyo Wizara hiyo imepata ni cha mshindi wa kwanza kwa mchezo wa karata ambapo Sudi Juma ni bingwa wa mchezo huo, kikobe cha pili ni cha mshindi wa tatu katika mchezo wa drafti ambapo Juma Mohamed ndiye ameikwakilisha vema Wizara katika mashindano hayo na hivyo kuifanya wizara hiyo kuwa na makombe hayo.
Aidha, katika mchezo wa riadha, mwanaridha Anita Brown ndiye aling’ara katika mbio za mita 100 na 200 wanawake kwa kuwa mshindi kwa kushika nafasi ya kwanza katika mbio hizo ambazo zilitimua vumbi katika kiwanja cha shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga.
Kaimu Katibu Mkuu Bw. Yakubu ameongeza kuwa uongozi wa Wizara hiyo wakiongozwa na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi na menejimenti nzima wapo bega kwa bega na wanamichezo wakati wote hatua inayodhihirisha kuwa hiyo ndiyo wizara yenye dhamana na kusimamia michezo nchini na amewataka viongozi wa klabu ya Wizara kuhakikisha michezo mingi inachezwa kuongeza wigo wa wanamichezo wengi zaidi wanashiriki mashindano hayo ambayo ni azma ya Serikali kuhakikisha watumishi wanashiriki michezo ili kuboresha afya zao na kuleta tija mahali pa kazi.
0 Comments