Header Ads Widget

”DUMISHENI USALAMA NA KUZINGATIA MAADILI YA JESHI LA POLISI”- RC SENDIGA



***************************

Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Rukwa wameagizwa kuhakikisha maisha ya watu na mali zao yanakuwa salama huku wakizingatia maadili ya kazi.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga leo (Alhamisi, Oktoba 13, 2022) wakati alipofanya kikao kazi na maafisa na askari waliopo makao makuu ya mkoa mjini Sumbawanga.

“Sitaki kuwa tayari kuona uonevu au vitendo vya rushwa ambavyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma. Askari akituhumiwa kwa ukiukaji maadili ni aibu kwa serikali” alisema Sendiga.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya usalama ya mkoa aliagiza kuwepo uwajibikaji kwa kuhakikisha upelelezi wa kesi za watuhumiwa ikiwemo wa ubakaji, ulawiti kwa watoto na mauaji zinafikishwa haraka mahakamani.

Sendiga alikemea tabia ya baadhi ya askari kuwaweka raia mahabusu kwa muda mrefu kinyume cha sheria hatua inayoleta malalamiko kwa wananchi kunyimwa haki zao.

Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa polisi wa mkoa na wilaya kuwa na utaratibu wa kusikiliza kero na shida za askari ili wapate utulivu kazini badala ya kuwakatisha tamaa.

Kwa upande Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Theopista Mallya alisema ataendelea kuhakikisha jeshi hilo linatimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ili kuleta utulivu na usalama kwenye jamii.

ACP Mallya aliongeza kusema jeshi hilo litaendelea kutekeleza maagizo na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo kutatua changamoto za askari.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI