UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Manispaa ya Moshi umefanya uchaguzi na kumchagua Sadath Ndibalema kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Katibu wa CCM wilaya ya Moshi mjini, Ibrahimu Mjanakheri alisema kuwa nafasi hiyo iligombewa na wanachama watatu ambao ni Anne Makata, Said Kifalali na Sadath Ndibalema.
Alisema kuwa, kura zilizopigwa ni 222 na kura zilizoharibika ni 2 ambapo Anne alipata kura 10 na Said alipata kura 64 huku Sadath akipata kura 146 na kuibuka kuwa mshindi.
Akizungumza kuwashukuru Wajumbe wa mkutano Mkuu wa Vijana wilaya, Sadath aliahidi kushirikiana na wanachama wa Umoja huo kuhakikisha chama kinasonga mbele.
Alisema kuwa, kwa kushirikiana na wanachama wa CCM atahakikisha kazi zote nzuri zilizofanywa na watangulizi wake anaziendelea ili kuhakikisha kuwa Jumuiya hiyo inasonga mbele.
Aidha aliwaahidi vijana wa Manispaa ya Moshi kuhakikisha anawasemea matatizo yao pamoja na kuhakikisha wanaunda vikundi vya ujasiriamali na kunufaika na mikopo ya Halmashauri ambayo ni asilimia nne ya mapato ya ndani.
Awali akifungua Mkutano Mkuu huo kabla ya kujiuzulu aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Issa Bulilo alisema kuwa, aliwataka viongozi waliochaguliwa kuongoza chama kuanzia ngazi ya matawi, Shina na kata kutambua kuwa jukumu lao kubwa ni kwenda kutafuta ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na ule uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Bulilo alisema kuwa, Wanachama wa CCM wanawaangalia viongozi waliowachagua kuwaongoza na kuwataka kutochukulia uongozi walioupata kama jambo la kawaida kwani hati ya chama ipo katika mabega yao.
Aidha alitumia pia nafasi hiyo kuwaasa vijana kutumia elimu waliyoipata katika kuisaidia Serikali ikiwamo kutafsiri kazi kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hasani na kuacha tabia ya kulalamika.
"Vijana ndio walinzi wa Chama cha Mapinduzi hivyo tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha chama kinaendelea kushika Dola na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi tutembeeni kifua mbele na kuzisemea kazi zinazofanywa na Serikali yetu" alisema Bulilo.
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya hiyo wilaya ya Moshi mjini, Arafat Mbiruka alisema kuwa, Jumuiya hiyo itaendelea kuwatetea vijana katika kuhakikisha wanapata haki zao ikiwamo mikopo ya Halmashauri.
Mbiruka alisema kuwa, Umoja huo katika Manispaa ya Moshi umeendelea kujipanga kuhakikisha CCM inaendelea kulitawala Jimbo la Moshi mjini pamoja na kata zake.
"Vijana ndio nguvu kazi ya chama na sisi kama vijana tutaendelea kumsemea vizuri Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Rais Samia Suluhu Hasani hasa kazi nzuri na kubwa ambazo amekuwa akizifanya na hatutamvumilia yeyote mwenyenia ya kumkwamisha katika utendaji kazi zake" alisema Mbiruka.
Mwisho..
0 Comments