Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WASHAURI wa wanafunzi katika vyuo vikuu nchini kupitia umoja wao (TACOGA) wameazimia kuendesha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari ikiwa ni moja ya mikakati ya kudhibiti vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinavyotokea kwenye vyuo vikuu.
Mwenyekiti wa TACOGA,Sophia Nchimbi akizungumza wakati wa kufunga mkutano mkuu wa mwaka wa TACOGA uliofanyika mjini Kigoma alisema kuwa wamekubaliana kwa pamoja kupitia umoja huo kuanza kuendesha mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari ili kudhibiti maadili na nidhamu za wanafunzi wakiwa bado katika elimu ya chini.
Pamoja na hilo aliwataka wazazi wa ngazi zote kuanzi shule za msingi,sekondari hadi vyuo vikuu kubeba jukumu la malezi ya watoto wao kwa kupata muda wa kukaa nao na kuwafundisha mienendo yenye maadili kwani itasaidia kuwakuza katika ustawi bora wenye maadili na nidhamu.
Akifunga mafunzo hayo Naibu Makamu Mkuu wa chuo kikuu huria cha Tanzania, Profesa Deus Ngaruko alisema kuwa ushauri kwa wanafunzi kwa sasa unapaswa kuwa taaluma na washauri wanapaswa kupata mafunzo ya kutosha kuweza kusimamia nafasi hiyo kwenye vyuo vikuu.
Alisema kuwa vyuo vikuu vina changamoto katika kuwalea na kuwasimamia wanafunzi wao kutokana na baadhi yao kuja na mambo ambayo yanapinganana taaluma na mienendo ya utoaji elimu kwenye vyuo vikuu hivyo ushauri kwa wanafunzi hawa unapaswa kusimamiwa kwa karibu ili kuwabadilisha na kuwafanya waweze kutimiza jukumu lao la kusoma.
Baadhi ya washauri wa vyuo vikuu nchini walisema kuwa maadili ya wanafunzi vyuo yameshuka na msingi wake haukuanzia vyuoni bali ulianzia kwenye jamii na masomo ya ngazi ya chini walipotoka ambao usimamizi wa maadili yao haukuwa wa kutosha.
Juma Hamisi mshauri wa wanafunzi kutoka Chuo kikuu cha Zanzibar alisema kuwa kazi kubwa inapaswa kufanywa kwa mashirikiano baina ya uongozi wa chuo, wazazi na jamii kwa jumla kwa sababu mambo mengi wanayofanya hayakuanzia vyuoni hivyo ni lazima kudhibiti mienendo na tabia huko wanapotoka.
0 Comments