Na Fadhili Abdallah,Kigoma
USIKILIZWAJI wa kesi na mashauri mbalimbali katika idara za mahakama mkoa Kigoma kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) umeleta mafanikio katika kusikilizwa kwa kesi nyingi, kutoa hukumu na kumaliza kesi ambazo zilikaa muda mrefu bila kumalizika.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Lameck Mlacha alisema hayo akifungua kikao kazi cha wajumbe wa kamati za kusukuma mashauri kwa ngazi za wilaya,mkoa na kanda ili kuhakikisha mpango mkakati wa usikilizaji wa mashauri kwa njia ya TEHAMA unatekelezwa kama ulivyokusudiwa bila kukwama.
Jaji Mlacha alisema kuwa tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa TEHAMA kwa ngazi za mahakama za wilaya, mkoa na Mahakama kuu kuanzia mwaka 2020 kumekuwa na ongezeko kubwa la usikilizaji wa mashauri hayo ambapo kwa mwaka huu Januari hadi Septemba Mashauri 1003 yamesikilizwa ukilinganisha na mashauri 37 yaliyosikilizwa mwaka 2020.
“Kanda imeweza kupunguza muda wa mashauri kukaa mahakamani hadi kufikia miezo mitano sawa na nchi ya Singapore ambayo mwaka 2015 ilikuwa na wastani wa mashauri kukaa mahakamani kwa siku 150 pekee,
nia yetu ni kuhakikisha hakuna kabisa kesi viporo vya kesi mahakamani,”alisema Jaji Mlacha.
Akizungumzia kuanzishwa kwa mfumo wa uendeshaji wa mashauri kwa njia ya Mtandao Mwakilishi wa Shirika la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) Mkoa Kigoma ,Peter Muriyuki alisema kuwa mpango huo umewezesha kusikilizwa kwa wakati kwa mashauri yanayohusu wakimbizi jambo ambalo ni muhimu katika mpango wa upatikanaji wa haki.
Muriyuki alisema kuwa UNHCR kama mdau itaendelea kushirikiana na idara ya mahakama mkoani Kigoma na wadau katika utoaji sheria na haki katika kuboresha miundo mbinu na utoaji haki ikiwemo kusaidia kuboresha mfumo wa TEHAMA kwa wadau mbalimbali ambao wanahusika kwenye suala la uendeshaji wa mashauri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha mawakili mkoa Kigoma, Daniel Rumenyera alisema kuwa mfumo wa TEHAMA umesaidia uendeshaji mashauri kwani wameweza kutumia mfumo huo kuendesha mashauri na wateja wao na mashahidi wakiwa kwenye ofisi yao ya wanasheria ambayo imewekewa mawasilinao na kuunganishwa na mfumo wa mahakama.
Rumenyela alisema kuwa hali hiyo imesaidia kupatikana kwa mashahidi kwa wingi,kurahisisha uendeshaji mashauri lakini pia imesaidia kupunguza gharama kwa wateja wao hasa wale wanaotoka mbalimbali na mahakama kuu.
Mkuu wa upelelezi jeshi la polisi wilaya ya Uvinza, Menas Temba alisema kuwa akiwa mjumbe wa kamati ya kusukuma mashauri ngazi ya wilaya na mkoa wamekuwa wakitimiza wajibu wao kuhakikisha tukio linafuatiliwa na upelelezi unakamilika kwa wakati na hasa wakati huu ambapo mfumo wa TEHAMA umekuwa na mafanikio katika kurahisisha uendeshaji mashauri.
Pamoja na hili amezungumzia malalamiko ya kuchelewa kwa upelelezi kunakosababishwa na polisi ambapo alibainisha kuwa umbali kutoka ofisi zao na mahali matukio yanapotokea lakini baadhi ya mashahidi ambao ndiyo muhimu kuelezea kuhusu tukio wanajificha hawataki kutoa ushirikiano ndiyo mambo yanayosababisha upelelezi, lakini wamejipanga kuhakikisha upelelezi hauwi kikwazo kwenye mpango huo
0 Comments