Afisa elimu sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoa Kigoma, Magreth Kilenza
Na Fadhili Abdallah,Matukio DaimaAPP,Kigoma
HALMASHAURI ya wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imeanza mkakati wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike katika shule za sekondari wilayani humo ili kukabiliana na mimba kwa wanafunzi sambamba na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa kike wilayani humo.
Afisa elimu sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoa Kigoma, Magreth Kilenza alisema hayo akizungumza wakati Mkurugenzi wa Afrika wa shirika la The Nature Conservancy (TNC),Ademola Ajagbe alipofanya ziara shule hapo kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la pili la wasichana linalojengwa shuleni hapo kwa ufadhili wa shirika hilowakati wa ukaguzi wa bweni la wanafunzi wa kike kwenye shule ya sekondari Lagosa.
Kilenza alisema kuwa moja ya mipango ambayo wameanza nayo ni kuweka kwenye bajeti ujenzi huo sambamba na kuandika maandiko mbalimbali kuomba ufadhili kutoka kwa wahisani ili kuwezesha ujenzi wa mabweni hayo.
Afisa elimu huyo alisema kuwa tafiti zao zimethibitisha kuwa ujenzi wa mabweni umekuwa suluhisho kubwa la kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa kike ikiwemo suala la mimba, ndoa za utotoni, utoro sugu na ufaulu duni kwani katika baadhi ya shule ambazo zina bweni kumekuwa na matokeo mazuri kitaaluma kwa wanafunzi wasichana.
Akitoa ushuhuda kuhusiana na ujenzi wa mabweni katika shule ya Sekondari Lagosa ulivyosaidia kuinua ufaulu na kukabili changamoto kwa wanafunzio wasichana Mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule hiyo, Kezia Herman alisema kuwa binafsi amenufaika kwa kiasi kikubwa na ujenzi wa mabwen I shuleni.
Kabla ya ujenzi huo alisema kuwa alikuwa akikumbana na vikwazo vingi ikiwemo kuchelewa shuleni kutoka na umbali kati ya shule na nyumbani na wakati wa mvua hali ni mbaya zaidi, ushawishi kutoka kwa wavulana na watu wenye kipato hali inayofanya wanafunzi wengi kupata ujauzito.
“Kwa sasa hali ni nzuri kwani tunapata muda miwngi wa kujisomea, kufanya majadiliano (Discussion) na wananfunzi wenzangu lakini tunafanya mambo yote kwa ratiba jambo ambalo limeongeza taaluma kwa wanafunzi hivyo tunahakika wengi wetu tutafanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha nne tunaomaliza mwaka huu,”Alisema Mwanafunzi huyo.
Mkuu wa shule ya sekondari ya Lagosa, Sophia Theobad alisema kuwa kabla ujenzi wa bweni hilo la wanafunzi kulikuwa na changamoto kubwa ya wanafunzi wa kike kumaliza kidato cha nne na kwa mwaka 2016 na 2017 ni wanafunzi sita walikuwa wanamaliza masomo huku wengine wakiacha shule kwa utoro sugu na mimba.
Mkuu huyo wa shule alisema kuwa wanafunzi wengi walikuwa wakiishi mbali na shule umbali wa kati ya kilometa 15 na 20 hivyo kuja na kurudi shule ilikuwa mzigo mkubwa kwao lakini tangu ujenzi wa bweni ufanyike mwaka 2019 shule imekuwa na mafanikio makubwa kwa wanafunzi wa kike kumaliza masomo.
Akizungumza na jumuia ya wanafunzi,wazazi na walimu wa shule hiyo Mkurugenzi wa Afrika wa Shirika la The Nature Conservancy (TNC), Ademola Ajagbe alisema kuwa shirika hilo limepokea kwa masikitiko changamoto ya wanafunzi wa kike wanaoshindwa kutimiza ndoto zao kwenye masomo na ndiyo maana imeamua kujenga mabweni hayo.
Ademola alisema kuwa ujenzi wa mabweni hayo mawili ni sehemu ya namna shirika hilo lilivyoguswa na changamoto hiyo na kutoa wito kwa wanafunzi hao kuongeza juhudi kwenye masomo yao ili kuvutia watu wengi zaidi kujitokeza kuongeza mabweni kwa wanafunzi hao.
0 Comments