NA HADIJA OMARY, MATUKIO DAIMAAPP, LINDI
JUMLA ya Watoto (182,312) walio chini ya miaka mitano Mkoani Lindi wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya Polio (matone) kupitia zoezi la kampeni ya kitaifa la utoaji wa chanjo hiyo kwa awamu ya tatu inayotarajiwa kufanyika kuanzia September 1 hadi 4, 2022 Nchi mzima.
Akizungumza Katika kikao cha kamati ya Afya ya msingi Mkoa juu ya kampeni ya kitaifa ya chanjo ya polio Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack aliwahakikishia wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama ambapo imekuwa ikitolewa kwa watoto kwa muda mrefu katika vituo vya kutolea huduma.
Hata hivyo Bi. Telack amehimiza wataalam kupeleka elimu kwa wananchi hasa wazazi ili watambue umuhimu wa chanjo hiyo ya polio itakayowakinga watoto wao na ugonjwa huo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Kheri Kyaga alisema kuwa Lengo la kampeni ya kitaifa ya chanjo ya matone ya polio ni kuhakikisha wanazuia uingizwaji wa ugonjwa wa polio nchini kulingana na mlipuko uliotokea Malawi na Msumbiji.
Alisema katika Kufanikisha lengo hilo ni muhimu kutoa kinga ya polio kwa watoto wote walio katika umri chini ya miaka mitano hata kama walishapata chanjo hiyo awali.
“Tathmini iliyofanyika na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi yetu ilionekana ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa polio endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa hii ni kutokana na mwingiliano wa wananchi baina ya Tanzania, Malawi na Msumbiji ” alifafanua Dkt. Kyaga.
Ameeleza kuwa kampeni hiyo ya chanjo itatolewa kwa kutumia mkakati wa kutembe nyumba kwa nyumba , pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile masoko, shule , misikiti, mashambani , vituo vya mabasi na makambi ya Wavuvi ambapo timu ya wachanjaji katika maeneo hayo kutoa huduma hiyo kwa siku nne.
“Kampeni hii itafanyika kwa utaratibu wa watoto wote kupewa chanjo majumbani na katika vituo vya kutolea huduma vilivyoandaliwa ambapo awamu ya kwanza ilifanyika tarehe 24-28 Machi, 2022 katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe huku Awamu ya pili ikitekelezwa mikoa yote hapa nchini (Bara na Zanzibar) kwa siku nne (4) kuanzia tarehe 28 Aprili mpaka 1 Mei, 2022”.
Kwa upande wake katibu wa Afya Mkoa wa Lindi, Richard Shabani alisema kuwa Ugonjwa wa polio ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi vijulikanavyo kwa jina la kitaalam kama poliovirus ambapo unaweza kumpata mtu yeyote katika umri wowote ila watoto huathirika zaidi Ambao umekuwa tishio kwa miaka mingi katika nchi nyingi duniani ikiwemo nchi ya Tanzania.
Alisema ugonjwa huo wa polio hautibiki na kwamba unaweza kuzuilika kwa kupata chanjo ya Polio pamoja na kuzingatia usafi wa mikono na usafi wa mazingira ikiwaemo matumizi ya sahihi ya choo bora.
“katika siku za hivi karibuni nchi ya Malawi ilitoa taarifa ya mgonjwa wa Polio mnamo tarehe 17 Februari, 2022. Mgonjwa huyu alipatikana katika mji mkuu wa Malawi-Lilongwe. Ambapo hata hivyo Mamlaka ya afya nchini Msumbiji pia mnamo tarehe 18 Mei 2022 ilitangaza mlipuko huo wa virusi vya polio baada ya kuthibitishwa kuwepo kwa ugonjwa katika jimbo la Kaskazini-Mashariki la Tete”.
Nae Mariam Saidi Mkazi wa Manispaa ya Lindi ameipongeza Serikali kwa kuchukua jitahada haraka za kukabiliana na ugonjwa huo kwa maslahi mapata ya Taifa.
“Ugonjwa huu wa Polio hautibiki zaidi ya kuzuilika , Mtoto akishapata polio hatoweza kupona tena atapata ulemavu wa kudumu mpaka kifo lakini kama wazazi tutajitokeza kuwachanja watoto wetu waliochini ya umri wa miaka mitano tunaweza kuwanusuru na ugonjwa huo" alisema Bi Mariam
0 Comments