Header Ads Widget

TBS YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZAKE

 


Na Hamida Ramadhan,Dodoma


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) linaendelea na juhudi za kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha huduma zake kwa lengo la kuwezesha biashara kwa dhumuni la kuinua uchumi wa viwanda kwa kuchagiza uzalishaji wa bidhaa salama na bora hapa nchini kama njia mojawapo ya kuchangia pato la Taifa.  


Mkurugenzi Mkuu wa shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt.Athumani Ngenya alieleza hayo Jijini Dodoma alipokuwa akieleza vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2022/23 alisema shirika lilianzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya sekta za Viwanda na Biashara ili kukuza uchumi wa Taifa. 


Aidha alisema kuwa Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Shirika limeandaa vipaumbele kwa kuzingatia Mpango mkakati wa Shirika wa mwaka 2021/2022- 2025/2026; Mpango mkakati wa Taifa (FYDPII) na Sera za Kisekta (wajasiriamali, biashara na viwanda).


VIPAUMBELE VYA SHIRIKA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023


Alisema kuwa Shirika limetenga kiasi cha TZS 9.9 Billioni kwa ajili ya kujenga jengo la maabara (Viwango House) katika miji ya kimkakati (Dodoma na Mwanza) ili kusogeza huduma za Shirika karibu kwa wateja na kuongeza ufanisi.


"Shirika limetenga kiasi cha TZS 2.7 Billioni kwa ajili ya kuimarisha ofisi saba za kanda (Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Mbeya) pamoja na ofisi za mipakani (Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea, Namanga, Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro,Sirari, Kabanga, Rusumo, Mtukula, Bandari ya bagamoyo, bandari ya Dar es salaam, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere- Dar, Bandari ya Tanga) kwa kuongeza wafanyakazi na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara sokoni ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama,


Shirika limetenga TZS 1.6 Billioni kwa ajili ya kuandaa viwango 630 vya kitaifa katika sekta mbalimbali ili kuwezesha biashara kwa kumpa uhakika mzalishaji wa kupata masoko ya ndani na nje, kumhakikishia mlaji wa mwisho usalama na ubora wa bidhaa atakayotumia ikiwa ni pamoja na kuweka ushindani sawia wa bidhaa katika soko,"alisema.


Pia alisema Shirika limetenga TZS 261 Millioni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za usajili wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi ili kuhakikisha wananchi wanatumia bidhaa zilizo bora na salama.


"Shirika limetenga TZS 581 Millioni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uthibitishaji wa mifumo ya kiutendaji ambapo kwa sasa TBS imepatiwa ithibati ya kufanya shughuli hiyo na mashirika yanaweza kuthibitishiwa ubora wa mifumo yao ya kiutendaji kupitia TBS. Hii itasaidia kuhakikisha wananchi wanapokea huduma zilizo bora,Shirika limetenga TZS 800 Millioni kwa ajili ya kufanya shughuli za kuhakiki ubora wa vipimo ili kuhakikisha usahihi wa majibu ya vipimo mbalimbali kutokea maabara, mahospitalini na viwandani na kupelekea watoa huduma au maamuzi kufanya maamuzi sahihi.


Shirika limetenga TZS 1.18 Billioni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini (PVoC) na baada ya kuwasili nchini (Destination Inspection) ili kuhakikisha nchi haiwi jalala la kupokea bidhaa zilizopigwa marufuku au hafifu,"alifafanua Ngenya.


TBS ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 3 ya mwaka 1975 na kuanza rasmi tarehe 16 Aprili 1976 ambapo ilipewa jukumu la kuratibu uandaaji wa viwango na kusimamia utekelezaji wake,TBS iliongezewa uwezo wa kusimamia shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora wa bidhaa kupitia Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009. 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI