NA CHAUSIKU SAID, MATUKIODAIMAAPP,
MWANZA.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima imeiagiza Chemba ya Wafanya Biashara (TCCIA) kuhakikisha wanatafuta eneo maalum kwa ajili ya kufanyia maonyesho ya Afrika Mashariki yanayofanyika kila mwaka.
Maagizo hayo ameyatoa wakati wa ufunguzi wa maonesho ya biashara ya Afrika Mashariki ya17 yaliyofayika katika viwanja vya mpira vya Nyamagana na kutoa siku 14 kwa wakuu wa wilaya ya Nyamagana na Ilemela kukaa chini kuangalia ni eneo lipi sahihi la kudumu litakalofaa kwa maonyesho.
"Tuamue huu ni uwanja wa mpira, kwa heshima ya Mwanza tunatakiwa kuwa na uwanja wa maonyesho, nataka tukubaliane mwakani hatutakuwa hapa tutakuwa na eneo la maonyesho linalokidhi mahitaji, kupita maonyesho haya tulitangaze jiji letu," amesema Malima.
Malima amesema kuwa atahakikisha anatafuta ufumbuzi na namna ya kutatua changamoto mbalimbali zilizotajwa na TCCIA ikiwemo ya wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kucheleweshwa kwenye mipaka wanapovusha bidhaa zao kuja kwenye maonyesho.
"Mwanza inatakiwa tuitangaze kama mji wa biashara na viwanda, wakuu wa wilaya hizi wakae ndani ya wiki mbili waje waniambie eneo gani tulitumie, haya maonyesho yana heshima kubwa yanatakiwa yalete watu lakini katika mazingira haya hatuwezi tunalipua," amesema Malima.
Makamu wa Rais Chemba ya Biashara upande wa viwanda, Clement Boko amesema wanajitahidi kuleta pamoja makundi ya wafanyabiashara, kilimo, wenye viwanda na ufugaji ili kuonyesha bidhaa zao.
“Tungeomba tuwe na eneo maalum kwa ajili ya maonyesho ambalo tuko tayari kushirikiana na taasisi za Serikali kuweka miundombinu ambayo itaturahisishia kuendesha maonyesho yetu kwa ufanisi," amesema Boko.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mugimi ametaja changamoto mbalimbali zinazoyakabili maonesho hayo ambazo ni kukosa sera ya kuwafanya wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo kujiunga na chemba, na utitiri wa kodi na ukiritimba wa baadhi ya taasisi za Serikali.
"Tunaiomba Serikali kutengeneza sera ya wafanyabiashara kujiunga na chemba ya wafanyabiashara, ianzishe sera ya sekta binafsi kutatua changamoto zinazoikabili na wafanyabiashara wanaotoka nje wapewe kipaumbele cha clearing kuwahisha bidhaa," amesema Mugimi.
0 Comments