Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kazi kubwa za utafiti wanazofanya. Pongezi hizo zimetolewa baada ya kupata maelezo kutoka kwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Mohammed Bashe (MB), wakati Mheshimiwa Rais Samia alipotembelea banda la Wizara ya Kilimo, katika kilele cha maonesho ya kitaifa ya wakulima yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Mheshimiwa Waziri Bashe amemweleza Rais Samia kuwa Wizara inajenga uwezo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia Kituo cha Mlingano ili kufanikisha ukusanyaji wa sampuli za udongo nchi nzima na kuzipima katika maabara ili kubainisha afya ya udongo na kuwashauri wakulima juu ya watumizi ya mbolea ili kuzalisha kwa tija.
Kuhusu kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula, Waziri wa Kilimo Bashe, amemueleza Mheshimiwa Rais Samia kuwa Wizara kupitia taasisi za TARI, ASA na TOSCI itazalisha mbegu bora za alizeti tani 5000 ambazo zitasambazwa kwa wakulima. Hatua hiyo itawawezesha wakulima kuzalisha alizeti nyingi ambayo itakamuliwa na kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.
Akizungumzia utafiti, Mhshimiwa Bashe alimweliza Rais kuwa Serikali yake imeongeza bajeti ya utafiti kutoka shilingi bilion 11 hadi bilioni 40 kwa mwaka wa fedha wa 2022/23. Alisema fedha hizo zitatumika kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa mzao mbalimbali nchini. Akizungumzia upatikanaji wa Mbegu bora za Mahindi Mheshimiwa Waziri Bashe alimweleza Rais Samia kuwa Wizara inaweka nguvu kuhakikisha mbegu bora ya mahindi ambayo ni chotara UH6303 inayofaa kwa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini itazalishwa kwa wingi ili iweze kusambazwa katika ukanda huo. Mheshimiwa Waziri alisema jitihada zinaendelea kuhakikisha mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na TARI zinazalishwa na ASA ili ziweze kupatikana kwa wakulima.
Waziri Bashe pia alimjulisha Mheshimiwa Rais Samia kuwa, ili kuwa na vyanzo vya nasaba za utafiti wakati wot, Wizara imeanza kukusanya na kuhifadhi mbegu za asili ili zisipotee kwa matumizi ya sasa na ya baadae.
0 Comments