NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara ya ufuatilia wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi pamoja na kufuatilia matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hasani katika kata ya Uru kusini.
Mbali na kukagua miradi hiyo ya maendeleo pia Mbunge huyo alitumia ziara hiyo kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya watu na makazi Agosti 23 mwaka huu pamoja na kufanya mikutano ya hadhara kwenye vijiji vya Rai na Shinga.
Katika ziara hiyo, Mbunge alifuatana na Diwani wa Kata hiyo Wilihad Kitali, Katibu wa CCM Wilaya Mahanyu, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali kutoka kata ya Uru Kusini, mwakilishi wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Moshi Eng Mchanga, Mwakilishi wa MUWSA, Flora na TANESCO Eng Freddy Robert.
Mbunge huyo alitumia nafasi ya ziara yake kufafanua mambo kadhaa yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika bajeti ya 2022/2023 na kupata fursa ya kusikiliza kero, kutatua kero, kupokea maoni na ushauri kutoka kwa Wananchi na kuhamasisha Sensa na shughuli za maendeleo.
Ziara hiyo ni utaratibu wa Mbunge aliojiwekea katika kujali wananchi wake kuwa kila akiwa likizo huwatembelea.
Katika ziara hiyo, Mbunge pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Kata ya Uru Kusini walipata fursa ya kutembelea Seminari ya Uru ambapo waliongea na viongozi wa shule, Kituo cha mafunzo ya awali ya waalimu cha Msamaria mwema kinachomilikiwa na KKT Dayosisi ya Kaskazini.
Aidha walitembelea kituo cha Malezi ya Mapadri Wazee kilichopo Mwenge kinachosimamiwa na Padri Charles Alleluya Mboya ambapo walipata fursa ya kusalimiana na mapadri wazee akiwemo Padri Lui Shayo mwenye umri wa miaka 103.
Mapadri hao kwa pamoja walimwomba Mbunge apeleke kilio chao cha kuitaka serikali iwapatie wazee wote nchini Pension na bima za uhakika za afya.
Katika ziara yake, Mbunge alizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mawela alipotembelea shule hiyo kukagua mradi wa ujenzi wa hosteli ya wasichana ambapo alipatiwa maelezo ya ujenzi wa hosteli hiyo kutoka kwa Mkuu wa shule msaidizi.
Akiwa shuleni hapo Mbunge aliwaomba watumishi wa shule hiyo wachape kazi na mbunge na Diwani watapambana kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora, ikiwemo utatuzi wa changamoto ya jiko la kupikia na ndipo alipozungumza na wanafunzi waliokuwa zamu na kuwaasa kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu kwa Walimu na Wazazi wao.
Katika ziara yake wananchi wa Kata ya Uru Kusini walieleza kufurahishwa na kasi ya utekelezaji wa baadhi ya ahadi za mbunge na diwani wao walizozitoa wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2020 hali iliyoanza kuwajengea matumaini makubwa kwa serikali ya awamu ya sita.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wananchi walieleza kuwa "Tumefarijika sana kupokea zaidi ya shilingi milioni mia saba toka kwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya cha Uru Kusini". Walisikika wakisema wananchi.
Baadhi yao wamesema kwamba: "Kipindi kilichopita tulimchagua mbunge lakini kwa kipindi chote cha miaka mitano hakuwahi kuonekana akirudi kuwasikiiza hali ya sasa ni tofauti kabisa". alisema mwananchi mmoja.
Wakiwasilisha kero zao wananchi wengi waliohudhuria mkutano katika kijiji cha Rau na Shinga walieleza kuwa kero yao kubwa ni ubovu wa barabara kama ile ya Kwa Mambo - Mama Ndizi - Kisawio na ile inayotokea Uru Seminary - Kisomboko hadi ukanda wa juu.
Walisema kuwa barabara zilizopo kwenye mtandao wa TARURA ni chache hali iliyomlazimu Mhandisi Mchanga toka TARURA alitoa ufafanuzi wa barabara zitakazokarabatiwa na kuchukua kero zilizowasilishwa na wananchi.
Mkazi mmoja wa Kata ya Uru Kusini alieleza kero ya Tumbili kuharibu mazao yao na kuwasababishia umaskini mkubwa ambapo Prof. Ndakidemi aliwaomba wasivunje sheria kwa kuwaua Tumbili hao kwani kero hiyo ameshaiwasilisha serikalini na inafanyiwa kazi.
Kero nyingine zilizowasilishwa ilikuwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi ya kijiji Shinga, kufufua soko la Molangi, Wateja wachache kuunganishiwa maji na Umeme na MUWSA na TANESCO, uchakavu wa Mifereji ya asili na kukosekana ajira kwa vijana.
Wawakilishi wa MUWSA na TANESCO walibeba kero zote na kuahidi kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa mbunge alihamasisha wananchi kuchangia miradi ya maendeleo kwenye kata kama vile kukarabati barabara za ndani, kujenga hosteli katika sekondari ya Mawela, kujenga ofisi katika kijiji cha Shinga na ofisi za Chama Cha Mapinduzi katika baadhi ya maeneo.
Mbunge aliwashauri vijana na akina Mama kujiunga katika vikundi vya wajasiamali ili wapatiwe mikopo ya halmashauri na kujikomboa kiuchumi. Aliwashauri vijana waavhane ta tabia ya kujihusisha na ulevi uliopindukia.
Akiongea katika mikutano hiyo Katibu wa CCM Wilaya Ramadhani Mahanyu amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali ya Rais Samia na kutoa ushirikiano ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili kwenye Kata yao kwa urahisi.
Mwisho...
0 Comments