Header Ads Widget

MWANAMKE WA MIAKA 60 AUWAWA NA WASIOJULIKANA

 


Na Mapuli Misalaba,Matukio DaimaAPP Shinyanga

Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Kabula Ngasa mwenye umri wa miaka 60, mkazi wa kijiji cha Nyida Kata ya Nyida katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga , ameuawa na watu wasiojulikana  kwa kukatawa panga sehemu mbalimbali za mwili wake.


Mwenyekiti wa kijiji cha Nyida Kidoto Maganga amesema kuwa, tukio hilo limetokea majira ya saa tatu usiku wa kuamkia leo Jumatatu, wakati Marehemu akiwa nyumbani kwake katika kijiji hicho.


Taarifa zaidi zinabainisha kuwa, watu waliofanya mauaji hayo walikuwa ni wawili ambao walifika nyumbani kwa Marehemu mapema na kujifanya wateja katika kibanda chake cha bidhaa dogodogo kilichopo hatua chache kutoka kwenye nyumba yake ambapo mwanzoni waliagiza Pipi na baadaye Soda na kuhudumiwa.


Baada ya dakika chache kupita walimtuma mjukuu wake anayesoma darasa la nne aliyekuwa naye kibandani kuwafuatia maji ya kunywa ndani, ambapo baada ya kurudi na maji walimpiga kwa ubapa wa panga hali iliyosababisha aanguke chini.


Alipoamka alikimbia kwa Mama yake ambaye anaishi jirani na kumweleza kinachoendelea, lakini inaelezwa kuwa Mama wa mtoto huyo aliogopa kutoka nje kwa vile Mume wake hakuwepo na hivyo watu hao wakatumia mwanya huo kumshambulia marehemu kwa Panga sehemu mbalimbali za mwili wake mpaka alipofariki dunia.


Mtoto wa Marehemu Jilala Pumula, amesema wakati mauaji ya Mama yake yakitokea, yeye alikuwa amekwenda kwenye ngoma kuuza Mahindi ya kuchoma.


Diwani wa kata ya Nyida Selemani Segereti , amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga George Kyando akibanisha kuwa,bado hajapata taarifa za tukio hilo kwa sababu yuko nje ya ofisi kikazi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI