Na Gabriel Kilamlya MBEYA
Ili kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto unaoukumba mkoa wa Njombe wenye asilimia 53 nchini Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kutoa elimu ya kilimo cha bustani za mbogamboga majumbani.
Katika maonesho ya kilimo Nane nane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya Halmashauri ya wilaya ya Njombe inatoa elimu hiyo kwa vitendo kupitia kilimo cha mbogamboga katika banda lao ambapo Afisa kilimo wa Halmashauri hiyo Bwana Ibrahim Fungo ambaye anashughulika katika kitengo cha kilimo cha mbogamboga anasema wanahamasisha wananchi wao kujikita katika kilimo hicho pamoja na kutumia kwa chakula ili kukabiliana na changamoto ya udumavu.
Baadhi ya wakulima wa mbogamboga hizo toka vijiji mbalimbali vya halmashauri hiyo akiwemo Theodomila Mwenda toka Nyombo wanasema kilimo hicho kinaweza kutumia eneo dogo kwa kulima aina tofauti za vitalu vya mboga mboga zinazoweza kumsaidia mwananchi kujipatia mboga kwa ajili ya chakula na hata kuuza.
Henry Kanyoka ni kaimu afisa Lishe halmashauri ya wilaya ya Njombe ambaye anasema dhana ya udumavu ni umri usioendana na urefu hivyo katika banda lao wanatoa elimu na kupima urefu,uzito kulinganisha na umri huku wakitoa ushauri wa namna ya kuendelea kuzingatia aina ya ulaji chakula.
Baraka Mwandute na Jackson Mwakarage ni baadhi ya wadau waliotembelea katika banda hilo kujifunza ambao wanakiri kuwapo umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya wataalam.
0 Comments