NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi, ameendelea na ziara zake kwa kuitembelea kata ya Mbokomu akiongozana na Diwani Rafael Materu na viongozi wa Chama na Serikali kwa ngazi ya vitongoji na kata, wataalamu kutoka TARURA, MUWSA, RUWASA, TANESCO na Afisa Maendeleo wa Kata.
Lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi ya maendeleo, kupokea kero za wananchi na kuhamasisha wananchi washiriki katika sensa itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu.
Mbunge alitembelea mradi wa ukarabati wa barabara ya Kiboriloni hadi Tema ambapo aliwakuta wakandarasi wakikarabati sehemu walizotengeneza vibaya na kushauriwa kuzirudia pia alikagua mradi wa maji wa Mbokomu unaosimamiwa na MUWSA ambapo alifurahi kujionea maji yakitoka kwenye mabomba.
Prof. Ndakidemi alifika shule ya sekondari ya Tema iliyokuwa imepokea ufadhili wa ujenzi wa matundu ya choo kutoka mfuko wa jimbo pamoja na shule ya Msingi Foyeni na kujionea ukarabati uliofanywa kwa nguvu za wananchi wa wafadhili wazawa.
Akiwa katika katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Tema, Mbunge aliwaasa wananchi wote wajitokeze siku ya Agosti 23 mwaka huu ili wahesabiwe.
Alisema, takwimu za sensa ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi wa Mbokomu yakiwemo makundi yenye uhitaji maalum kama vile, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee.
"Kujua idadi kamili ya watu na makundi mbalimbali itarahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo" alisema Prof. Ndakidemi.
Mbunge aliwaambia wananchi kuwa katika Bajeti ya mwaka 2022/2023 fedha za kutosha zimetengwa kutekeleza miradi ya elimu, afya, maji, barabara, na kilimo ikiwepo fedha za ruzuku ya mbolea, miche bora ya ya kahawa na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji.
Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge Ndakidemi aliwashauri wananchi wa Mbokomu washiriki kikamilifu kwenye miradi ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuchangamkia miche bora ya kahawa itakayotolewa na Serikali na fedha ya ruzuku ya pembejeo.
Aliwashauri vijana kujiunga kwenye vikundi na kujilimia mbogamboga ili wajipatie kipato kwani kufanya hivyo watajiajiri na kuongeza mzunguko wa fedha na kuwashauri pia wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu wamtumie vyema Afisa Maendeleo wa Kata ya Mbokomu ili awasaidie kupata mikopo inayotolewa na halmashauri kwa makundi haya.
Wakiwakilisha kero zao, wananchi wengi walilalamikia kero ya ubovu wa barabara hasa kipindi cha mvua katika maeneo yote ya kata ya Mbokomu.
Wananchi walieleza kutokuridhika na ukarabati unaoendelea katika barabara ya Kiboroloni hadi Tema kwani mkandarasi ametumia kifusi kilicho na asilimia kubwa ya udongo badala ya changarawe.
Kero hii ilithibitishwa na Mwakikishi wa TARURA kwani walimwelekeza mkandarasi arudie kazi iliyofanyika chini ya kiwango kwenye maeneo korofi.
Wakiwakilisha kero za idara ya afya, wananchi walimweleza Mbunge kwamba katika zahanati zote za Kata ya Mbokomu, hakuna huduma za mama na mtoto huku pia hakuna Maabara hata moja na watu husafiri kwenda mjini Moshi kupata huduma hizo kwa gharama kubwa.
Kero ingine kubwa iliyowasilishwa na wananchi ni uchakavu mkubwa wa majengo ya shule za msingi ambayo mengi yalijengwa kabla ya Tanzania kupata uhuru.
Mwakilishi wa Tanesco aliwaambia wananchi kwamba hali ya umeme katika kata ya Mbokomu inaridhisha na changamoto zolizoripotiwa katika kijiji cha Korini Kusini na Tema zitafanyiwa kazi.
Baada ya kuwasikiliza wananchi, Mbunge na Diwani Rafaeli Materu walijibu hoja mbalimbali na waliahidi kufikisha kero zote kwenye mamlaka husika.
Kwa pamoja waliwashukuru wananchi na wafadhili mbalimbali wanaosaidia kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Mbokomu.
Mwisho.
0 Comments