NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amefanya ziara ya kutembelea Kata ya Kibosho Kati.
Mbunge Ndakidemi aliandamana na Diwani wa Kata hiyo Bahati Mamboma, viongozi wa Chama ngazi ya Wilaya na Kata, wataalamu kutoka TARURA, RUWASA na Tanesco akiongozwa na meneja wa Kanda ya Kaskazini Mhandisi Fedgrace Ezekiel Shuma akifuatana na mkuu wa Tanesco Kilimanjaro Mhandisi Abdulrahman Nyenye.
Katika ziara hiyo, Mbunge Ndakidemi alikagua miradi ya ujenzi wa vyoo katika shule za msingi Uri na Otaruni na kujionea ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji katika shule ya msingi Uri.
Ukarabati wa vyoo hivi ulifadhiliwa na mfuko wa jimbo wa Mbunge akiwa Kibosho Kati, Mbunge alijionea juhudi za Tanesco kusambaza umeme kwenye makazi ya watu.
Baada ya ziara ya kutembelea miradi, Prof. Ndakidemi alipata fursa ya kuhudhuria msiba katika kijiji cha Uri na kuwapa wafiwa mkono wa pole.
Akimkaribisha Mbunge kuongea na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Maua, Diwani wa Kata ya Kibosho Kati, Bahati Mamboma aliainisha miradi iliyotekelezwa katika Kata yake.
Miradi hiyo ni kama ule wa kuboresha upatikanaji wa umeme katika Kata, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa vyoo na madarasa katika shule za sekondari na msingi na uboreshaji wa miundombinu ya maji safi na salama.
Alisema kuwa kero yao kubwa ni ubovu wa barabara za ndani na uchakavu wa mifereji ya asili.
Akiongea na wananchi, Prof. Ndakidemi aliwahimiza wananchi wote wajitokeze Agosti 23 mwaka huu ili wahesabiwe.
Alisema, takwimu za sensa ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi wa Kata ya Kibosho Kati yakiwemo makundi maalumu kama vile, wazee, vijana, wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Prof. Ndakidemi aliishukuru serikali iliyo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta za Elimu, miundombinu ya barabara, maji, Afya na umeme.
Aliwaomba wananchi wawe walinzi wa miradi hiyo kwa kuitunza kwani ni yao na wasipofanya hivyo watakosa huduma.
Wakiwakilisha kero zao, wananchi wengi walionyesha kukerwa na ubovu wa barabara za ndani hasa ile inayoanzia KNCU - Maua - Marambo ambapo pamoja na umuhimu wa barabara hiyo, bahati mbaya ni kwamba haipo kwenye mtandao wa TARURA.
Mbunge alifurahi kusikia kuwa wadau wa maendeleo wa kijiji cha Maua walikuwa wameshachangisha shilingi milioni 6 ili kukarabati barabara hiyo ambapo alichangia laki tano kuwaunga mkono.
Katika mkutano huo, wananchi walisikitishwa na spidi ndogo ya utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa wakati wa kampeni.
Waziri mkuu aliahidi kuwa serikali ingekamilisha barabara ya International School - Kwa Raphael - Kibosho Shine kwa kiwango cha lami baada ya uchaguzi.
Mwakilishi wa Tarura katika mkutano huo Mhandisi Mchanga alisema TARURA itaendelea kuziweka barabara za Kibosho Kati katika mipango yao ya ujenzi na Ukarabati, ikiwepo hiyo ya kukamilisha kwa kiwango cha lami.
Kero nyingine kubwa iliyotawala mkutano wa Mbunge ni ya wananchi kutokutaka kupewa huduma ya kupata maji safi na salama kutoka RUWASA.
Pamoja na maelezo ya kina ya mwakilishi wa RUWASA, Mbunge Ndakidemi aliwaambia wapiga kura wake kwamba swala la kusambaza maji ni la kisheria, na hawawezi kukiuka hiyo sheria iliyotungwa na kupitishwa na Bunge.
"Jukumu la kusambaza maji katika kata ya Kibosho Kati kisheria ni la RUWASA kwa kushirikiana na Jumuiya ya watumia maji ya vijiji tisa vya Kibosho na siyo la kikundi cha OMA kama walivyokuwa wanafikiri niwaombe RUWASA wajikite kuwaelimisha wananchi kuhusu mabadiliko haya ya kisheria ili kupunguza migogoro" alisema Prof. Ndakidemi.
Kero ya Matumizi mabaya ya shamba la ushirika linalomilikiwa na wanaushirika wa Kimasio na Kirima boro iliibuliwa katika mkutano huo na Emanuel Mboro.
Mboro alisema kuwa viongozi wamekuwa na tabia ya kuuza shamba la ushirika kinyemela bila kushirikisha wamiliki jambo linalosababisha sintofahamu kubwa.
Alimwomba Mbunge asaidie kufuatilia ambapo aliahidi kulifuatilia, kwani kero hiyo ilijitokeza kwenye mkutano wake wa Kata ya Kirima.
Wakiongea katika mkutano huo, wawakilishi wa Tanesco wakiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kaskazini Mhandisi Fedgrace Shuma waliwahakikishia wananchi kuwa kwa kushirikuana na Diwani na Mbunge, TANESCO itatatua changamoto zote za umeme zinazoikabili Kata ya Kibosho Kati.
Katibu wa Umoja wa Vijana Wilaya Melkiory Pantaleo aliwaomba wananchi wa Kibosho Kati waiunge mkono Serikali ya Rais Samia kwani makubwa anayofanya kwenye taifa hili yanaonekana.
Akiwa anafunga kikao, Mwenyekiti wa CCM Kata Edward Mallya amemshukuru Rais Samia kwa miradi mikubwa ndani ya Kata yao pamoja na kumshukuru Mbunge na Diwani kwa ushirIkiano mkubwa baina yao unaopelekea wananchi kupata maendeleo.
Mwisho.
0 Comments