Na Amon Mtega, Songea
WAZIRI wa Katiba na Sheria ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Mkoani Ruvuma Dkt Damas Ndumbaro amewataka wakazi wa Jimbo hilo kuacha tamaa ya kuuza mahindi yote kwenye kaya zao kutoka na kuwepo kwa bei kubwa ya zao hilo jambo ambalo linaweza kusababisha familia kuwa na upungufu wa chakula.
Dkt Ndumbaro ameutoa wito huo wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa Jimbo hilo kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika baadhi ya kata ikiwemo kata ya Mshangano na Shuleyatanga Manispaa ya Songea huku mikutano hiyo ikiwa imepambwa na burudani mbalimbali za wasanii.
Mbunge Dkt Ndumbaro ambaye amefanya ziara kwenye baadhi ya kata hizo kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali za wananchi pamoja na kuhamasisha suala la Sensa na makazi August 23 mwaka amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya wakazi wa Jimbo hilo kuwa na tabia ya kuuza mahindi yote ndani ya kaya zao na mwisho wa siku familia inakuwa na njaa jambo ambalo halitakiwi.
Amesema kuwa katika msimu huu mahindi yanauzwa bei kubwa ya sh.600 hadi sh.620 kwa kilo moja jambo ambalo baadhi yao wanaingiwa tamaa ya kuuza mahindi yote bila kuacha akiba ya chakula ndani ya kaya zao.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo amewataka wakazi wa Jimbo hilo kwenda kuhesabiwa Sensa pamoja na kutambua kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kupatiwa ruzuku kwenye mbolea jambo litamfanya mkulima kupunguziwa garama za pembejeo hiyo.
Kwa upande wake meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano awali akimkaribisha Mbunge huyo aweze kuzungumza na hadhara hiyo amesema kuwa Manispaa hiyo itaendelea kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali inayokuwa imeibuliwa na Wananchi pamoja na miradi inayoagizwa na Mbunge wa Jimbo hilo na miradi ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM yenye kurasa 303 ambayo utekelezaji wake unaendelea.
Nao wakazi wa kata ya Mshangano walimshukuru Mbunge huyo pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi ya kuwaletea maendeleo kwenye kata hiyo na Jimbo kwa ujumla huku wakimuahidi Mbunge huyo kuendelea kushirikiana na Serikali yao ili waweze kupatiwa maendeleo zaidi.
0 Comments