Header Ads Widget

MBUNGE ANNE KILANGO ARIDHISHWA NA UJENZI WA VITUO VYA AFYA NA ZAHANATI KATIKA JIMBO LA SAME MASHARIKI

 


NA WILLIUM PAUL, SAME.


MBUNGE wa Jimbo la Same mashariki mkoani Kilimanjaro, Anne Kilango Malecela ameridhishwa na ujenzi wa kituo cha Afya cha Miamba na kituo cha Afya Mtii pamoja na zahanati za Kirongwe na Ntambwe.


Mbunge huyo ambaye yupo jimboni kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya watu na makazi Agosti 23 mwaka huu.



Alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inaboresha huduma za afya pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi.


“Nimekuja kukagua ujenzi wa vituo vyetu vya afya vilivyopo kata ya Mtii pamoja na Miamba pamoja na vituo vya zahanati katika kata ya Bwambo na Mpinji serikali imetoa fedha katika vituo vya afya na zahanati wananchi wamechangishana sasa nataka kuona matumizi ya fedha hizo” alisema Anne Kilango.



Akizungumzia ujenzi wa kituo cha Afya Miamba, Mtendaji kata, Janeth Mbwambo alisema kuwa, mradi huo wa kituo cha afya ulianza Januari 15 mwaka huu ambapo majengo manne yanatarajiwa kujengwa pamoja na kichomea taka.


Janeth aliyataja majengo hayo kuwa ni jingo la wagonjwa wa nje (OPD), jingo la maabara, jengo la mama na mtoto na jengo la upasuaji ambapo majengo mawili yapo katika hatua ya ukamilishaji na ujenzi wa majengo yote yanatarajiwa kukamilika Septemba 30 mwaka huu na wananchi wanaanza kuhudumiwa.



“Kwa sasa tumeshapokea madaktari watatu kwa ajili ya kutibu wananchi katika kituo hicho kinachotarajiwa kuhudumia wananchi wa vijiji vinne vilivyopo ndani ya kata hiyo pamoja na kata jirani za Mpinji, Bwambo na kata ya Lugulu” alisema Mtendaji kata Janeth.



Aliongeza kuwa, mpaka sasa wameshapokea milioni 350 za ujenzi hivyo wamebakisha milioni 150 ili kuhakikisha kituo hicho kinakamilika na wananchi wanapata huduma ya afya karibu kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu wa kilomita 8 kufuata huduma ya afya katika hospitali ya Bwambo.



Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela aliipongeza Serikali ya chama cha Mapinduzi kwani kwa jimbo zima lilikuwa na kituo cha Afya kimoja ambacho ni Ndungu hivyo kupatikana kwa kituo hicho cha Afya Miamba kitakapokamilika pamoja na Mtii kutafanya jimbo hilo kuwa na vituo vya afya vitatu.




Alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa muda mfupi ambao ameongoza na kufanya mambo makubwa kwa wananchi wa jimbo la same mashariki katika sekta ya Afya na barabara.



KITUO CHA AFYA MTII.

Mbunge Anne Kilango Malecela alifika kata ya Mtii na kujionea ujenzi wa kituo cha afya na ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), ambapo serikali ilitenga jumla ya Milioni 279.



Akitoa taarifa ya ujenzi kwa Mbunge, Kaimu Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Benjamin Charles alisema kuwa, kituo hicho kilipokea milioni 29 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), na Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la maabara, kichomea taka pamoja na jengo la mama na mtoto ambapo mpaka sasa wametumia milioni 79.



Dkt. Charles alisema kuwa mpaka sasa jengo la mama na mtoto limeshafikia asilimia 38 na jengo la maabara limefikia asilimia 60 ambapo kukamilika kwa kituo hicho kitapelekea wananchi waliokuwa wakienda zahanati ya Kanza na hospitali binafsi ya Bombo kupata huduma hapo.



Aidha alisema kuwa, kwa sasa Jengo la wagonjwa wa nje linafanya kazi lakini wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa tiba, uhaba wa watoa huduma na madaktari na wauguzi pamoja na ukosefu wa dawa kwa asilimia 60.


Aidha alisema kuwa, ujenzi wa majengo hayo umechelewa kukamilika kutokana na mfumo wa manunuzi katika halmashauri kufungwa pamoja na tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi.



Naye Mbunge Anne Kilango aliwataka wasimamizi wa ujenzi wa kituo hicho kuwa makini kuhakikisha ujenzi unakwenda kwa kasi ili wananchi waweze kunufaika na fedha ambazo serikali yao imeweka.


Aidha Mbunge huyo alitoa kitanda cha kisasa kwa ajili ya wakinamama wajawazito kujifungulia huku pia akiendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kujitolea nguvu kazi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.



Katika zahanati za Kirongwe na Ntambwe zilizopo kata ya Mpinji na Bwambo ambapo ujenzi wake upo katika hatua ya msingi, Mbunge huyo alifurahishwa na jinsi ambavyo wananchi wanajitolea michango yao kuhakikisha zahanati hizo zinajengwa ambapo aliwaunga mkono kwa kutoa fedha taslimu milioni 1 pamoja na kuahidi kutoa mifuko ya saruji 100.




Mwisho…

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI