Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka vijana kuacha kufanya vitendo viovu na kushinda mitandao muda mrefu kuangalia mambo yasiyofaa badala yake wafanye kazi.
Kauli hiyo, ameitoa jijini Dar es Salaam wakati akifungua Tamasha la Kwanza la Kitaifa la Utamaduni na kuwataka watu wote wanaojihusisha na vitendo viovu vinavyokiuka misingi ya maadili waache mara moja na badala yake kuishi kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania.
Aidha, amesisitiza kuwa kuwa familia ni kitovu cha makuzi na malezi kwa watoto na vijana, ambapo amesema familia ni asasi ya msingi na muhimu katika mfumo wa jamii na hivyo inaweza kuendeleza maadili, malezi na urithishaji wa utamaduni wetu wa Kitanzania.
Amesema kuwa, walezi na wazazi wanatakiwa wajifunze kutilia maanani malezi ya watoto kwa kutenga muda wa kukaa na watoto na vijana na siyo kuziachia shule peke yake, washirikiane na Serikali, taasisi za dini na wadau wengine, kukemea mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu.
Aidha, amewataka vijana wote wa Kitanzania waache kuendekeza tabia ya kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii kwa kusoma au kuangalia mambo ambayo hayaongezi thamani ya maisha yao na badala yake watumie muda huo kufanya kazi, hivyo watumie mitandao kutafuta maarifa yanayofaa na tujikite zaidi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.”
“Kwa kuwa maadili ni chimbuko la uzalendo na utu wetu, ninaitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuongeza jitihada katika kuandaa programu za elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuthamini mila na desturi zetu, pamoja na uzalendo, ili tutengeneze kizazi kinachozingatia maadili mema. Tusikubali kamwe kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni.”
Amesema kuwa, wamekua wakishihudia baadhi ya vitendo viovu vingi kama vile kuongezeka kwa vitendo vya watoto kuwauwa wazazi wao, ulawiti, wanawake kuuwawa na waume zao, ubakaji hususani kwa watoto na wanafunzi, watoto na vijana kutowaheshimu watu wazima hususani katika vyombo vya usafiri na kutumia lugha zisizofaa wanapozungumza na watu wazima, uvaaji wa mavazi yasiyo na stara hususani kwa wasichana na wavulana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa tamasha hilo, Waziri Mkuu amesema tamasha hilo limetokana na agizo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa akiwa mkoani Mwanza tarehe 8 Septemba, 2021 kwenye Tamasha la Utamaduni, ambapo Rais Samia alielekeza yafanyike matamasha ya utamaduni ya namna hii nchi nzima.
"Naiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, iandae mwongozo wa jinsi gani matamasha haya yataendeshwa. Pia ninaiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na wadau ambao wanaandaa matamasha ya Utamaduni"
Amesisitiza kuwa, wadau wahakikishe wanaishirikisha Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wanapoandaa matamasha yao wahakikishe wizara husika inafahamu. “Si vema mdau unaandaa tamasha huku wizara yenye dhamana na utamaduni haifahamu kabisa au inafahamu dakika za mwisho
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema tamasha hilo ambalo linafanyika kwa siku tatu lilianzia jana Julai Mosi, 2022 litamalizika kesho Julai 3, 2022, limeandaliwa mahsusi katika wiki ya kuelekea siku ya Kiswahili Duniani ambayo kilele chake ni Julai 7, 2022.
Tamasha hilo litachagizwa na shughuli mbalimbali zikiwemo mashindano ya ngoma za kitamaduni na vyakula vya asili pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali za kitamaduni, ambapo Kauli mbiu ya tamasha hilo inasema “Utamaduni wetu; tujiandae kuhesabiwa, kazi iendelee.
Amesema moja ya matokeo tarajiwa la tamasha hilo ambalo limeshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ni kuwepo kwa hamasa kubwa nchini ya kupenda, kuhifadhi, kulinda, kuendeleza mila na desturi ambazo ndio msingi wa maadili na utambulisho wa Taifa kwa ujumla.
Awali, Waziri Majaliwa alipokea matembezi ya utamaduni ambayo yalihusisha wananchi kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao walipita wakiwa katika magari ya wazi huku kila mkoa ukionesha na kucheza ngoma za utamaduni za mkoa husika.Tamasha hilo limejumuisha matembezi ya kiutamaduni (road carnaval) katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam.
0 Comments