Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma
MTAKWIMU Mkuu wa Serikali Dkt Albina Chuwa amewatoa hofu Wananchi Kuhusu usiri wa taarifa zitakazokusanywa katika zoezi la Sensa ya Watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu huku akibainisha kuwa hakuna takwimu zitakazotumika vibaya kwa wasimimizi wa zoezi hilo .
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini hapa Dkt Albina Chuwa alisema kabla ya kufanya zoezi hilo wasimamizi wa zoezi la Sensa ya Watu na makazi watapewa kiapo maalumu cha kutunza siri za watu watakaokwenda kuwahesabu katika Kaya .
"Niwatake Wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa kwa kutoa taarifa sahihi kwa Maendeleo ya taifa letu kwani takwimu zitakazopatikana zitakwenda kuisaidia Serikali kujua inawahudumiaje Wananchi wake,"
Na kuongeza Kusema"Niwatoe hofu Sheria za takwimu zinaeleza kuwa kwa wasimamisi wa zoezi hilo la sensa watakaovujisha siri Sheria kazi zitachukuliwa dhidi yao kwa kufungwa kifungo cha miaka miwili jela, au faini ya Shilingi milion 2 au vyote kwa ujumla.
“Niwatoe hofu watanzania kuwa serikali imedhamilia kufanya zoezi hili kwa umakini mkubwa tutahakikisha kila kitu atakachokisema mwananchi inakuwa ni siri kati yake na karani na kwa atakayekiuka sheria itafuata mkondo wake,”alieleza.
Aidha akieleza maandalizi ya Sensa ya watu na makazi Dkt Albina alisema mpaka Sasa maandalizi yamefikia asilimia 87 ambapo kwa sasa Ofisi ya taifa ya Takwimu (NBS) imeanza kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa sensa katika ngazi ya Mkoa.
Baada ya mafunzo hayo washiriki watakaofaulu watakuwa na wajibu wa kwenda kufundisha wasimamizi na makarani wa sensa ambao watapata nafasi baada majina yao kutangazwa katika maeneo waliyoomba.
Alisema mafunzo hayo yatafanyika Kwa siku 21 na yatahusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Waratibu wa sensa ngazi ya wilaya,pamoja na wawakikishi kutoka vyama vya watu wenye ulemavu.
Alieleza zoezi la maandalizi linaenda vizuri, baada ya kukamilisha mafunzo ya wakufunzi katika ngazi ya Taifa hatua inayofuata ni mafunzo katika ngazi ya mkoa ambao yameanza rasmi leo katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar ambapo mafunzo haya yatafanyika Kwa siku 21.
"Baada ya kukamilika Kwa mafunzo hayo Julai 29 mwaka huu yatafuata mafunzo katika ngazi ya wilaya ambapo kutakuwa na makarani,wasimamizi wa maudhui,na wasimamizi wa TEHAMA itahusisha washiriki walioomba nafasi hizo na kukidhi vigezo na kufanya usahili," alisema Dkt Albina.
Hata hivyo Dkt,Albina alisema katika tathmini ambayo wameifanya hivi karibuni wamebaini kuwa asilimia 97 ya wananchi wamekubali kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu
"Hii ni hatua kubwa ukilinganisha na mwaka 2012 katika kipindi kama hichi ni asilimia 80 ya wananchi ambao walikuwa wamekubali kuhesabiwa,".
Na kuongeza "Tuko makini katika suala la sensa tutahakikisha hadi kufikia siku ile ya sensa tutakuwa tumekamilisha hatua zote zinazohitajika na kwa sasa ukiangalia ratiba yetu imebana sana hatuna muda wa kupoteza,”alisema Dkt Albina






0 Comments