**********
NA AMON MTEGA, MBINGA.
WAKULIMA 58 wa Zao la Kahawa wa Kijiji cha Mahenge kata ya Litembo Wilaya ya Mbinga ambao hawakulipwa malipo ya mauzo ya zao hilo kwenye chama cha msingi cha mahenge (Mahenge AMCOS)wanatarajiwa kulipwa malipo hayo mapema Agosti mwaka huu kabla ya kuingia msimu mwingine.
Akizungumza mwenyekiti wa chama hicho Julius Mbunda kwenye mkutano wa hadhara uliyoandaliwa kwaajili ya kutatua changamoto za wadai hao huku ukisimamiwa na Afisa tarafa wa Mbuji Salma Kipande amesema kuwa chama kimejipanga kuhakikisha wakulima hao wanalipwa mapema Agosti mwaka huu ili kusiwepo na changamoto hiyo tena.
Mwenyekiti Mbunda amefafanua kuwa sababu za wakulima hao kushindwa kulipwa malipo yao kwa wakati ni kufuatia deni ambalo walilikopa benki kwaajili ya kununulia mashine mbili za kukobolea kahawa katika Kijiji cha Mahenge na Kijiji cha Langandondo wakati wakitumia AMCOS moja na kuwa kabla ya halijalipwa deni hilo Kijiji cha Langandondo kilikuwa kimefanikiwa kupata AMCOS yake hivyo malipo ya kahawa yalipoingia benki ,yalikatwa kwa jina la wakulima wa Mahenge kutokana na mkopo huo kuwa na jina la Mahenge.
Amefafanua kuwa AMCOS hiyo ambayo inasoko la kuuzia kahawa ndani ya Nchi na Nje ya Nchi ambao wadau wao wa soko la Nje ni wakutoka Ujerumani wakitumia kampuni ya Parterkaffee iliingiza fedha za malipo kwa wakulima wote kutokana na mkataba waliyowekeana hivyo makato yalifanyika benki kutokana na deni hilo.
Amesema kuwa kampuni hiyo ya Ujerumani licha ya kulipa fedha zote kwa makubaliano ya mkataba lakini bado imekuwa ikitoa fedha kama bakishishi ya mauzo ya kahawa (Socialpremium) kwaajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya AMCOS hiyo kama ya ujenzi wa shule ya Sekondari inayojengwa katika kijiji cha Mtama Kitongoji cha mwembe Halmashauri ya Mbinga mjini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho Gerida Ndunguru amesema kuwa anafurahishwa na mwelekeo mzuri wa utatuaji wa changamoto ya malipo hayo kwa wakulima hao jambo ambalo litaondoa malalamiko kwa baadhi yao.
Mmoja wa wakulima katika kijiji hicho Karistus Hyera ambaye yeye alishapatiwa malipo ya kahawa tangu awali amesema kabla ya mkutano huo walikuwa hawajui lini wenzao watapatiwa malipo hayo lakini sasa wameshatambua .
Aidha Afisa tarafa wa Mbuji Salma Kipande amewataka viongozi kujenga tabia ya kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali za wakulima ili kwenda sambamba na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha changamoto za jamii zinatatuliwa kwa wakati.
Hata hivyo afisa tarafa huyo alimpongeza mwenyekiti wa AMCOS hiyo pamoja na bodi yake kwa kuibua miradi mbalimbali ambayo itakuwa msaada kwenye chama hicho huku akiwataka waendelee kuwa wamoja.









0 Comments