MKUU wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amemtaka Katibu Tawala wa na ofisa elimu wa mkoa huo kuweka mkakati wa kuendeleza michezo ili iweze kuchukua nafasi yake.
Ameyasema hayo Mjini Kibaha kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) wakati akifunga michezo ya Umoja wa Michezo Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) Mkoa huo.
Kunenge amesema kuwa mikakati ikiwemo ya viwanda imefanikiwa sasa mikakati hiyo ihamishiwe kwenye michezo kwani mkoa una vipaji vingi ambavyo vinapaswa kuendelezwa.
Amesema kuwa safari ya ustawi wa michezo tayari imeanza na tunataka ichukue nafasi yake kwa kuwekeza kuanzia ngazi za chini hivyo lazima kuwe na utaratibu mzuri ili kufikia hayo.
"Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa anatoka mkoa wa Pwani hivyo lazima tuonyeshe uweze ili kumuunga mkono kwa Pwani kuwa na hamasa kubwa ya michezo,"amesema Kunenge.
Aidha amesema kuwa atakuwa mlezi wa timu hiyo ili kuhakikisha inafanya vizuri kwa kushirikiana na wadau wa michezo na kuhakikisha shule mbili za Michezo za Zogowale na Fukayosi na nyingine mbili zitakazoongezeka na kuwa nne zinapata vifaa ili kuendeleza vipaji.
Awali ofisa elimu mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kuwa Mashindano hayo ya siku nne yameshirikisha jumla ya Halmashauri tisa za mkoa huo na jumla ya wanamichezo 900 walishiriki ambapo wamechaguliwa 120 kwa ajili ya kuwakilisha mkoa huo.
Mlaki amesema kuwa baada ya wachezaji hao kuchaguliwa wataingia kambini kwa siku nne ambapo wataondoka kwenda Tabora kwenye Mashindano hayo kitaifa yatakayoanza Julai 30 hadi Agosti 8 na ujumbe wa Mashindano ya mwaka huu unasema Takwimu Sahihi ni Msingi wa Mipango bora ya Taifa Shiriki Sensa ya Watu na Makazi kwa Maendeleo yetu.
Mwisho.






0 Comments