Na Gift Mongi, Moshi
Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu vijana kazi na ajira Patrobas Katambi amezitaka taasisi zinazoshughulikia masuala ya kazi zilizopo ofisi ya waziri mkuu kuungana wakati wa utekelezaji wa majukumu ili kuondoa usumbufu kwenye kampuni wakati wa ukaguzi.
Katambi alitoa agizo hilo katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa usalama mahali pa kazi uliofanywa na kiwanda cha sukari cha TPC kama mwajiri na chama cha wafanyakazi (TASIWU) mjini Moshi.
Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni mfuko wa fidia kwa wafanyakazi(WCF)wakala wa usalama mahali pa kazi (OSHA)mfuko wa hifadhi ya jamii(NSSF)mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma(PSSF)ambapo zinatakiwa kuwa na timu moja katika kwenda kufanya ukaguzi ambapo itaondoa usumbufu.
"Kukiwa na timu moja itarahisisha utoaji wa huduma lakini pia itaenda kuondoa usumbufu wa mara kwa mara kwani hawa wote majukumu yao yanashabihiana hivyo ipo haja ya kufanya hivyo"alisema
Kuhusiana na mkataba huo usiosainiwa na pande zote yaani mwajiri na mwajiriwa alisema kampuni nyingi zimekuwa zikishindwa kufanya vizuri kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri kati ya mwajiri na wafanyakazi wake jambo ambalo alisema kwa TPC limekuwa Ni kinyume na ndio maana wameweza kusonga mbele katika uzalishaji.
"Mna bahati ya kipekee ambapo mwajiri wenu TPC anawaruhusu hadi kujiunga katika vyama vya wafanyakazi ambapo wengine wamekuwa wakikataa jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu na kanuni zinavyoelekeza"alisema
Alisema ipo haja kwa sasa kampuni nyingine kuja kujifunza TPC namna wanayoishi na wafanyakazi wao ili kwenda kutumia ujuzi katika kampuni zao ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro mahali pa kazi
Ofisa mtendaji mkuu (utawala) wa kiwanda cha TPC Jaffary Ally alisema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiboresha maslahi ya wafanyakazi wake kadri faida inabopatikana ambapo mwaka jana bilioni 2.3 zilitolewa kwa wafanyakazi ili kugawana faida.
"Wafanyakazi wetu hapa TPC mwaka jana tuliweza kugawana nao faida ya kile walichozalisha ambapo bilio 2.3walipewa hii maana yake ni kuwa nao wanatakiwa kupata faida ya kile walichokizalisha"alisema Jaffary
Katika hatua nyingine alisema TPC imekuwa ikirudisha faida yake kwa jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara,shule,zahanati,kusomesha watoto wanaotoka familia duni na miradi mingine,
Alisema TPC pia wamekuwa wakiwasomesha watoto wa wafanyakazi wake lakini pia kuwapatia huduma bure ikiwemo umeme ambao unatokana na makapi ya miwa kiwandani hapo hivyo kupunguza gharama za maisha.
Jacob Mshana ni mwenyekiti wa taifa chama Cha wafanyakazi (TASIWU)alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni kielelezo kuwa TPC inawajali wafanyakazi wake na kuwa hali hiyo kwa kiwango kikubwa hupunguza migogoro mahali pa kazi.
Mwisho.






0 Comments