Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam
Waajiri wote nchini Tanzania wametakiwa kuajiri maafisa rasilimali watu na maafisa mahusiano wanye uweledi na kazi yao ambao wataweza kumshauri vizuri na kumwambia ukweli kiongozi wake katika namna bora ya kiutendaji Ili kuepusha mrundikano wa madeni kwa wafanyakazi wake.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Vijana Ajira na watu wenye ulemavu) Potras Katambi wakati alipokua akielezea hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na wafanyakazi, madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri nchini.
Amesema kuwa, kutokana na ukaguzi unaoendelea kufanyika katika maeneo ya kazi umeonesha kuwa maafisa rasilimali watu na maafisa mahusiano wanashindwa kuwashauri vizuri viongozi wao na kusababisha kampuni kupata matatizo ikiwemo mrundikano wa madeni pamoja na kutowapatia stahiki wafanyakazi wao ikiwemo kutopeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
"Kuna baadhi ya maafisa rasilimali watu hawawambii ukweli mabosi zao, hawatimizi wajibu wao, wanaona wakiongea ukweli watafukuzwa kazi basi wanaishia kukaa kimya na wakati mwengine kuwashauri vitu ambavyo sio sahihi, muda mwengine huweza hata kumfanyia mwenzie fitina akizani ndio atapendwa yeye na kiongozi wake"amesema Naibu Waziri Katambi.
Aidha, amesema kuhusu suala la bima ya Afya, NSSF na pensheni kwa wastaafu jambo hilo lipo kwa mujibu wa sheria, hivyo waajiri wote wametakiwa kuwasajili na kuchangia wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF na WCF) wakiwemo wafanyakazi na madereva, hivyo Serikali itaendelea kufuatilia waajiri hao Ili kuhakikisha wanatekeleza sheria ipasavyo.










0 Comments