MICHEZO ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mkoa wa Pwani imeanza kutimua vumbi huku timu kutoka Wilaya za mkoa huo zikichuana vikali kwenye michezo mbalimbali.
Mashindano hayo ambayo yanafanyika kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi Halmashauri tisa zinachuana kwenye michezo hiyo inayofanyika kila mwaka.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisa michezo wa mkoa wa Pwani Grace Bureta amesema kuwa Mashindano hayo yatakuwa ya siku tatu hadi Agosti 24 mwaka huu.
Bureta amesema baada ya hapo itachaguliwa timu ya mkoa itakayoundwa na wachezaji 120 kwenda kwenye Mashindano ya Taifa yatakayofanyika mkoani Tabora.
Kwa upande wake Mwalimu wa mchezo wa mpira wa kengele unaohusisha wachezaji wenye ulemavu uoni hafifu Miriam Tegete amesema amewaandaa vizuri wachezaji wake ili kufanya vizuri kwenye michezo hiyo.
Katika baadhi ya matokeo mpira wa pete timu ya Kibaha Mji imeshinda kwa magoli 14-11 dhidi ya Kisarawe, mpira wa mikono Bagamoyo imeshinda kwa magoli 9-0 dhidi ya Chalinze.
Mpira wa wavu Kibaha Mji imeshinda seti 2-0 dhidi ya Bagamoyo kwa upande wa soka Kibaha Halmashauri imeifunga Mkuranga 3-2.







0 Comments